USHINDI wa mabao 3-0 ilioupata dhidi ya Stand United muda mchache uliopita, umeifanya Azam FC kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, imekaa kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 26 ikiizidi Simba pointi tatu, ambayo ipo nyuma mchezo mmoja itakaocheza kesho Jumamosi dhidi ya Ndanda.

Azam FC ilionyesha kabisa kuwa inataka kuibuka kideda baada ya kufanya shambulizi kali dakika ya pili tu, lilotokana na mpira wa faulo uliopigwa na Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, ambao ulimkuta Joseph Mahundi aliyepiga kichwa kilichopaa juu ya lango.

Jududi za Azam FC zilizaa matunda dakika ya 21 baada ya kiungo Salmin Hoza, kuiandikia bao la uongozi akifumua shuti kali nje kidogo ya eneo la 18 lililojaa wavuni huku kipa wa Stand United, Frank Muhonge, akiishia kutazama linavyojaa kimiani.

Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, ambapo ingizo la mshambuliaji Bernard Arthur, aliyeingia dakika ya 33 kuchukua nafasi ya Idd Kipagwile, lilizaa matunda baada ya kuipatia bao la pili Azam FC dakika ya 64, akianza kumchambua kipa wa Stand kabla ya kutupia mpira wavuni akimalizia pasi safi ya Yahya Zayd.

Hilo ni bao la kwanza kwa Arthur kwenye mechi rasmi ya mashindano tokea asajiliwe na Azam FC akitokea Liberty Professional ya Ghana katika usajili uliopita wa dirisha dogo.

Beki wa kushoto Bruce Kangwa, alihitimisha ushindi huo kwa kuifungia Azam FC bao la tatu kwa jitihada binafsi baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Stand United na kuingia kwenye eneo la hatari kabla ya kupiga shuti lililomshinda kipa.

Mara baada ya ushindi huo, kikosi cha Azam FC kesho Jumamosi mchana kinatarajia kuelekea visiwani Zanzibar tayari kwenda kutetea ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ilioutwaa mwaka huu.

Azam FC iliyokuwa Kundi A sambamba na Simba, Mwenge, Jamhuri (zote za Pemba) na URA ya Uganda, itafungua pazia la michuano hiyo kehsokutwa Jumapili kwa kukipiga dhidi ya Mwenge mchezo utakaoanza saa 10.30 jioni.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Himid Mao (C), Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris, Stephan Kingue/Salum Abubakar dk 61, Joseph Mahundi, Salmin Hoza, Yahya Zayd, Enock Atta/Shaaban Idd dk 81, Idd Kipagwile/Bernard Arthur dk 33