KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Ijumaa itakuwa ikisaka uongozi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) pale itakapochuana na Stand United katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Azam FC itakuwa ikisaka kukaa kileleni kutokana na kujikusanyia pointi 23 sawa na Simba, hivyo ushindi wowote wa matajiri hao utawafanya kufikisha pointi 25 na kuwasubiri wekundu hao ambao watacheza keshokutwa Jumamosi dhidi ya Ndanda.

Kikosi cha Azam FC kipo vizuri kuelekea mchezo huo na usiku huu kimemaliza maandalizi ya mwisho kabla ya kuwavaa Stand, wachezaji wote wakiwa na morali kubwa ya kuweka kuibuka na pointi zote tatu ili kuzidisha mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo.

Wachezaji majeruhi

Azam FC itaendelea kukosa huduma za wachezaji wake watano, beki Daniel Amoah, winga Joseph Kimwaga na washambuliaji Shaaban Idd na Mbaraka Yusuph, ambao bado ni majeruhi wakiendelea na programu za mwisho za kurejea dimbani.

Mwenendo wa ligi

Wakati Azam FC inayodhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents ikiwa ni miongoni mwa timu mbili kileleni baada ya kushinda mechi sita na sare tano, Stand United yenyewe ipo mkiani ikijikusanyia pointi saba tu, zilizotokana na ushindi mechi moja, sare nne na kupoteza mara tano.

Rekodi zilipokutana

Kihistoria tokea Stand United ipande daraja mwaka 2014, Azam FC imecheza nayo mechi sita za ligi, matajiri hao wakishinda asilimia 99.5 ya mechi hizo baada ya kushinda mara tano na kupoteza mchezo mmoja.

Stand United haijawahi kufunga bao lolote wala kuibuka na ushindi ilipocheza na Azam FC ndani ya viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, ushindi pekee iliyoupata ilikuwa ni katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga msimu uliopita ikishinda bao 1-0.

Katika mabao 11 yaliyofungwa baina ya timu hizo, Azam FC imefunga mabao 10 na moja lililobakia likifungwa na Stand, huku robo tatu ya mabao yote ikiyafunga kwenye Uwanja wa Azam Complex (mabao saba).

Mchezo wa mwisho zilipokutana kwenye uwanja huo msimu uliopita, Azam FC ilishinda mabao 2-0.

Itakumbukwa kuwa, Azam FC wikiendi iliyopita imetoka kuifunga Area C United ya Dodoma mabao 4-0 katika mchezo wa raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).