BAADA ya kuinyoa mabao 4-0 Area C United usiku wa kuamkia leo, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, hivi sasa akili zao zote wamezielekeza kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Stand United utakaofanyika Desemba 29, mwaka huu.

Azam FC imetoa dozi hiyo kali katika mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), mabao yaliyowekwa kimiani na kiungo Salmin Hoza, Nahodha Msaidizi Agrey Moris, mshambuliaji Yahya Zayd na winga Enock Atta, ambaye alitengeneza pia mabao matatu ukiacha alilofunga.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aristica Cioaba, alisema amefurahishwa na matokeo waliyoyapata timu yake na kufunguka kuwa kwa sasa wanaangalia mchezo ujao dhidi ya Stand utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

“Ninafuraha kubwa baada ya wachezaji kuingia kwenye mchezo wakiwa na umakini, walimuheshimu mpinzani, hili ni jambo zuri wachezaji walitambua kuwa michuano hii mipya mechi za kwanza zinakuwa ngumu kama hautakuwa na umakini kwa asilimia kubwa na kuingia uwanjani kwa ajili ya kushinda mchezo.

“Ninafuraha tumeshinda mchezo hivi sasa ni vizuri kusubiria mchezo ujao wa ligi (Stand United) tuna muda wa wiki moja ya kujiandaa kwa ajili ya mchezo huo,” alisema.

Aidha katika kujiandaa vilivyo na mchezo huo, kikosi hicho leo Jumapili jioni kimefanya mazoezi kama kawaida kwa benchi la ufundi kuwagawa wachezaji kwenye makundi mawili, la kwanza likwia na wachezaji waliocheza mechi ya jana ambao walipewa programu ya kurudisha mwili katika hali ya kawaida (recovery program) na wengine waliobakia wlaiendelea programu ya kawaida ya mazoezi.

Kikosi hicho kinatarajia kupumzika kesho kwenye sikukuu ya Krismasi kabla ya kurejea mazoezini Jumanne saa 12.00 jioni kuendelea na mazoezi ya kujiandaa kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya Stand United.

Mkono wa Krismasi kwa mashabiki

Katika hatua nyingine, kwa niaba ya uongozi wa Azam FC na wachezaji, Ciaoba alichukua fursa hiyo kuwatakia kila la kheri mashabiki na wapenzi wa timu katika kusherehekea vema sikukuu ya Krismasi inayoadhimishwa kesho Jumatatu na Jumanne na Wakristo duniani kote.

“Jana niliona baadhi ya mashabiki wa Azam FC wamekuja uwanjani kwenye mchezo na kusapoti timu na wamerudi nyumbani wakiwa na furaha, nawashukuru sana mashabiki kwa kuiamini timu.

“Nataka niwaambie inakuja Krismasi, napenda kuwaambia mashabiki wote wa Azam FC na familia ya Azam Kheri ya Krismasi furahieni sikukuu hii ya Krismasi na mrejee baada ya Krismasi na tuendelee kufanya kazi pamoja kwa ajili ya hapo baadaye,” alisema.

Azam FC inarejea kwenye mchezo wa raundi ya 12 ya ligi ikiwa inakabana koo na Simba kwenye kilele cha msimamo wa ligi wote wakiwa na pointi 23 lakini matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex wakizidiwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.