KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeanza vema michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada kuipiga Area C United mabao 4-0, mchezo uliomalizika usiku huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam FC ilionyesha kuwa imedhamiria kuibuka na ushindi katika mchezo huo baada ya kufanya shambulizi kali dakika ya pili tu kufuatia Enock Atta kuwazidi ujanja mabeki wa Area C na kupiga mpira mzuri wa faulo uliomkuta Paul Peter, aliyepiga kichwa kilichogonga mwamba wa pembeni kabla ya mabeki kuokoa hatari hiyo.

Azam FC kwa ushindi huo mnono, ni kama imetoa zawadi ya Sikukuu ya Krismasi kwa mashabiki wake kutokana na mchezo huo kuwa wa mwisho kwa timu hiyo kabla ya maadhimisho ya sikukuu hiyo kufanyika keshokutwa Jumatatu na Jumanne.

Alikuwa ni kiungo Salmin Hoza, aliyeanza kufungua mlango wa mabao kwa Azam FC dakika ya 17 baada ya kupiga shuti kali nje kidogo ya eneo la 18 akimalizia mpira wa faulo aliotengewa na winga Enock Atta Agyei, ambaye leo alicheza kama beki wa kulia.

Huku ikicheza vema kwa kasi na mpira wa pasi, Azam FC ilijipatia bao la pili dakika ya 34 lililofungwa na na Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, aliyepiga kichwa kikali kilichomshinda kipa akimalizia mpira wa kona uliochongwa na winga Enock Atta.

Mshambuliaji Yahya Zayd, naye aliweza kuitumia vema kona nzuri nyingine iliyochongwa na Atta dakika ya 41 akiiunganisha kwa kichwa na kuipeleka mapumziko Azam FC ikiwa na uongozi wa mabao 3-0.

Atta aliyekuwa kwenye kiwango kizuri akitoa pasi tatu za mabao, alihtimisha ushindi mnono wa Azam FC kwa kuifungia bao safi la nne dakika ya 53 kwa shuti la chini akimalizia mpira safi wa krosi uliochongwa na beki wa kushoto Bruce Kangwa.

Kwa matokeo hayo, Azam FC imefanikiwa kusonga kwa raundi ya32 bora ya michuano hiyo na sasa inasubiria mpinzani wake mwingine wa kupangwa naye kwenye raundi hiyo.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Himid Mao/Swaleh Abdallah dk 54, Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue/Bernard Arthur dk 77, Joseph Mahundi, Salmin Hoza, Paul Peter/Wazir Junior dk 61, Yahya Zayd, Enock Atta