MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Mbaraka Yusuph, anatarajia kukaa nje ya dimba kwa muda wa wiki mbili baada ya kupata mshtuko mdogo kwenye goti lake la mguu wa kushoto.

Mbaraka amegundulika na tatizo hilo baada ya kufanyiwa uchunguzi leo asubuhi kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo jijini Cape Town, Afrika Kusini.

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mara baada ya mshambuliaji huyo kumaliza mapumziko hayo ya wiki mbili ataruhusiwa rasmi kuanza mazoezi madogo madogo.

“Mbaraka ameonwa na daktari Nickolas ambaye ni daktari bingwa wa magoti pamoja na nyonga na matokeo ya vipimo yanaonyesha kwamba amepata mshtuko tu wa mguu sio kama taarifa tulizozipata awali kwamba ameumiza meniscus (washa).

“Kwa hiyo Mbaraka atapumzika kwa muda wa wiki mbili na baada ya wiki mbili atafanya mazoezi madogo madogo na ataweza kurudi kwenye ushindani kama kawaida,” alisema.

Mwankema aliongeza kuwa mara baada ya matibabu, nyota huyo anatarajia kurejea nchini keshokutwa Jumapili kuuguza majeraha hayo.

Yusuph amekwenda nchini humo kwa matibabu sambamba na Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Abdulkareem Amin ‘Popat’, ambaye ndiye ameshughulikia taratibu zake zote za matibabu.

Aidha, nyota huyo alipata majeraha hayo akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ iliyokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika nchini Kenya wikiendi iliyopita.