KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumamosi itaanza kibarua chake cha kwanza kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Fedaration Cup) kwa kumenyana na Area C United ya Dodoma.

Mtanange huo wa raundi ya 64 ya michuano hiyo utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku, ambapo Azam FC imejinasibu kuichapa timu hiyo na kusonga mbele kwa raundi ijayo.

Kuelekea mchezo huo, Azam FC ilicheza mechi nne za kirafiki wakati Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) iliposimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika wikiendi iliyopita nchini Kenya, ambapo ilitoka sare mmoja dhidi ya Friend Ranagers (1-1) na kushinda mitatu walipokipiga na Mvuvumwa (8-1), Villa Squad (7-1) na Polisi Tanzania (3-1).

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, alisema kuwa wachezaji wote wana ari kubwa na anaimani kubwa wataibuka na ushindi dhidi ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL).

“Mimi nafikiri mechi unapocheza na mtu wa chini mechi inakuwa ngumu kwa sababu mtu wa chini wakati mwingine haji na staili yoyote anahakikisha wewe hupati nafasi ya kucheza kwa hiyo anajituma katika hali zote ili aweze kukutoa nishai.

“Lakini sisi tumejipanga na hilo tumeshacheza mechi kama hizo tunajua namna gani ya kuzicheza ili kuhakikisha mchezo tunaurahisisha na tunapata ushindi uliokuwa mzuri,” alisema

Azam FC inayodhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, itaingia kwenye mchezo huo ikiwakosa wachezaji wake wanne ambao ni majeruhi, beki Daniel Amoah, mshambuliaji Mbaraka Yusuph, pamoja na wale wa muda mrefu, winga Joseph Kimwaga na mshambuliaji Shaaban Idd.

Msimu uliopita kwenye michuano hiyo Azam FC iliishia hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa na Simba bao 1-0, kwenye mchezo ambao matajiri hao walicheza pungufu kwa takribani dakika 75 baada ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kuonyeshwa kadi nyekundu.