MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mbaraka Yusuph, ameshatua jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa matibabu ya goti lake la mguu wa kushoto baada ya kuumiza washa (meniscus).

Yusuph amekwenda na Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Abdulkareem Amin ‘Popat’, ambaye ndiye atashughulikia taratibu zake zote za matibabu akiwa nchini humo.

Baada ya kuwasili, mshambuliaji huyo kesho Ijumaa saa 2 asubuhi kwa saa huko (saa 3 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki) anatarajia kuonana na daktari wa Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo jijini Cape Town tayari kuanza uchunguzi wa tatizo lake.

Nyota huyo alipata majeraha hayo akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ wakati ikicheza na Libya kwenye mchezo wa michuano ya Kombe la Chalenji ulifanyika nchini Kenya Desemba 3 mwaka huu.