MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mbaraka Yusuph, anatarajia kuondoka nchini kesho Jumatano jioni kuelekea jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa uchunguzi wa goti lake la kushoto baada ya kuumiza ‘meniscus’ (washa).

Yusuph alipata majeraha hayo akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ wakati ikicheza na Libya kwenye mchezo wa michuano ya Kombe la Chalenji ulifanyika nchini Kenya Desemba 3 mwaka huu.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, alisema kuwa tayari uongozi wa timu hiyo wameridhia na atakwenda sambamba na Makamu Mwenyekiti, Abdulkarim Nurdin ‘Popat’, atakayekuwa akishughulikia taratibu zake zote za matibabu.

“Mbaraka atakwenda kufanyiwa kwanza uchunguzi zaidi baada ya kupata uchunguzi wake na kupata majibu kwamba ni kitu gani kinamsumbua zaidi wao ndio watajua kuwa Mbaraka anahitaji operesheni au atapewa tiba mbadala,” alisema.

Bernard Arthur mambo safi

Katika hatua nyingine, Jaffar alithibitisha kuwa tayari timu hiyo imepokea vibali vya kufanya kazi nchini kwa mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Bernard Arthur, ambaye sasa ni rasmi ataruhusiwa kucheza kwenye mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Area C United ya Dodoma utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

“Bernard Arthur yupo huru kucheza mashindano yote ambayo yanahusu Azam FC kwa maana kwamba taratibu za kupata vibali vyake vya kufanya kazi nchini zimekamilika, sisi Azam FC tunamatumaini kwamba kwa kushirikiana na wenzake atatoa mchango mkubwa na vilevile kuweza kuhakikisha kuwa safu yetu ya ushambuliaji itazidi kuchangamka zaidi,” alisema.

Arthur amesajiliwa akitokea Liberty Professional ya Ghana kwa mkataba wa miaka miwili, ambapo hadi sasa ameshafunga mabao matatu kwenye mechi za kirafiki alizocheza akifunga la kwanza dhidi ya Friends Rangers katika sare ya bao 1-1 kabla ya kutupia mawili, Azam FC ilivyoilaza Villa Squad mabao 7-1.