KATIKA kumalizia maandalizi yake katika kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kinatarajia kukipiga dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumanne saa 1.00 usiku.

Huo ni mchezo wa nne wa kirafiki kwa timu hiyo baada ya mapumziko hayo kupisha michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika jana Jumapili nchini Kenya, ilianza kwa kutoka sare na Friends Rangers (1-1) kabla ya kuzichapa Mvuvumwa (8-1) na Villa Squad (7-1).

Akizungumzia programu ya mchezo huo dhidi ya timu hiyo ya polisi, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, alisema watautumia kama sehemu ya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Area C United, Ligi Kuu na Kombe la Mapinduzi.

Azam FC itafungua pazia la michuano ya Kombe la Shirikisho msimu huu kwa kukipiga dhidi ya timu hiyo kutoka mkoani Dodoma inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL), mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumamosi hii saa 10.00 jioni.