TIMU ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 13 (Azam U-13) imeibuka mabingwa ya michuano ya Kombe la Chipkizi kwa vijana wa umri huo baada ya kuichapa Express Academy kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya bao 1-1.

Mashindano hayo yanaandaliwa na Future Stars Academy ya mkoani Arusha, ambapo Azam FC ndio mara ya kwanza kushiriki ikiwa na vikosi vipya ilivyoviunda hivi karibuni.

Azam U-13 iliweza kufanya kweli na kupenya hadi robo fainali ikiifunga timu ya CTID bao 1-0, kisha nusu fainali ikaibugiza Moi Educational Centre ya Ghana mabao 5-0 kabla ya fainali kuifunga Express.

Azam U-11 yenyewe haikufanikiwa kuingia robo fainali, lakini katika raundi za awali iliifunga Icons Football Academy ya Kenya (2-1) kabla ya kupoteza kwa bao 1-0 ilipocheza na Moi Educational Centre (1-0) na kutoka suluhu na Elite Soccer Academy.

Mara baada ya michuano hiyo kumalizika, vikosi hivyo vya Azam FC vinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu.