KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya kweli usiku huu baada ya kuipiga Villa Squad mabao 7-1 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Huo ulikuwa ni mchezo wa tatu wa kuwaweka fiti wachezaji baada ya mapumziko ya Ligi Kuu ya Vodacoma Tanzania Bara (VPL) kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inayohitimika kesho Jumapili nchini Kenya.

Katika hatua nyingine benchi la ufundi la Azam FC chini ya Mromania Aristica Cioaba, lilikuwa likiutumia mchezo huo pia kuangalia kikosi kitachocheza kwenye mtanange ujao wa raundi ya 64 ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Area C United ya Dodoma utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Desemba 23 mwaka huu.

Mabao ya Azam FC katika mchezo huo yamefungwa kiustadi na Joseph Mahundi, Bernard Arthur waliofunga mawili kila mmoja, huku Yahya Zayd, Bruce Kangwa na Wazir Junior, nao wakikamilisha ushindi huo kwa kufunga moja kila mmoja.

Ulikuwa ni usiku mzuri wa winga Mahundi, ambaye alionyesha kiwango kizuri akicheza kwa spidi wakati wa kushambulia pamoja na kusaidia ukabaji timu inapokuwa haina mpira.

Kikosi cha Azam FC

Razak Abalora/Mwadini Ally dk 46, David Mwantika/Abdul Omary dk 78, Bruce Kangwa/Hamimu Karim dk 78, Daniel Amoah, Agrey Moris/Oscar Masai dk 74, Salmin Hoza/Frank Domayo dk 64, Stephan Kingue/Braison Raphael dk 64, Joseph Mahundi/Masoud Abdallah dk 64, Bernard Arthur/Wazir Junior dk 56, Yahya Zayd/Idd Kipagwile dk 56, Enock Atta/Salum Abubakar dk 56