TIMU za vijana za Azam FC chini ya umri wa miaka 11 na 13, zimeanza vema michuano ya Kombe la Chipkizi kwenye mechi zao walizoanza kucheza jana Ijumaa katika Uwanja wa TGT mkoani Arusha.

Azam U-11 iliyoko Kundi C kwa vijana wa umri huo kwenye michuano hiyo, imeanza kwa kuichapa Icon Football Academy ya Kenya mabao 2-1 kabla ya Azam U-13 kupata ushindi wa chee baada ya mpinzani wake Viraj International School (Kenya) kutotokea uwanjani.

Baada ya mpinzani wake kuingia mitini, kikosi cha Azam U-13 kilitumia mwanya huo kucheza mchezo wa kirafiki na timu kutoka Kenya ya Consolate FC na kufanikiwa kuibugiza mabao 11-1.

Michuano hiyo inayoandaliwa na kituo cha kukuza vipaji cha mkoani Arusha cha Future Stars, itaendelea tena leo Jumamosi kwa timu za Azam FC kucheza tena, ambapo Azam U-13 itakipiga na wenyeji Future Stars saa 7.50 mchana kabla ya kushuka tena dimbani saa 11.10 jioni kumenyana na Elite Soccer Academy.

Aidha Azam U-11 nayo itavaana na Syokimau Academy saa 4.00 asubuhi, kisha itakipiga na Soccer Africa ya Kenya saa 6.40 mchana kabla ya kumaliza na Moi Edu Cent B saa 10.40 jioni, mechi zote zikipigwa kwenye viwanja vya TGT mkoani humo.