KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumamosi kitaendelea na programu ya mechi za kirafiki ambapo kinatarajia kukipiga dhidi ya Villa Squad ya Kinondoni katika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Huo utakuwa ni mchezo wa tatu wa kirafiki kati ya minne iliyoko kwenye programu ya benchi la ufundi wakati huu wa mapumziko ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya.

Mechi mbili zilizopita, Azam FC ilianza kutoka sare bao 1-1 na Friends Ranger kabla ya juzi kuichapa Mvuvumwa United ya Kigoma mabao 8-1.

Mbali na kuitumia kuwaweka fiti wachezaji, pia benchi la ufundi limekuwa likiwajumuisha kikosini wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kutosha ya kucheza katika mechi za ligi.

Mara baada ya mechi za kirafiki, Azam FC inatarajia kucheza mechi ya kwanza ya ushindani dhidi ya Area C United ya Dodoma Desemba 23 mwaka katika mchezo wa raundi ya 64 ya michuano ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup), utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Msimu huu, kikosi hicho kimepanga kutwaa taji la michuano hiyo baada ya kulikosa kwa misimu miwili mfululizo tokea lianzishwe, mara ya kwanza msimu wa 2015-2016 ikifungwa mabao 3-1 na Yanga katika fainali kabla ya msimu uliopita kuishia nusu fainali kufuatia kufungwa bao 1-0 na Simba.