MICHUANO ya Ligi ya Vijana ya Azam chini ya umri wa miaka 15 (Azam Youth League U-15) imemalizika juzi ikishuhudiwa JMK Park ikiibuka mabingwa baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 24.

Wenyeji Azam FC iliyojikusanyia pointi 18 ilishika nafasi ya pili katika ligi hiyo iliyochukua wiki 10, huku zilizofuatia zikiwa ni Rendis (16), Bom Bom (11), Tanzanite (9) na Millenium ikifunga dimba baada ya kuzoa pointi nne tu.

Tunakuletea stori muhimu kwa mfumo wa namba kuhusu ligi hiyo;

13.9: Namba hiyo ni uwiano wa umri wa wachezaji wa Azam FC, ambayo ndio timu iliyoweka rekodi ya kuwa na wachezaji wengi wadogo miongoni mwa timu sita shiriki za michuano hiyo.

15: Ni idadi ya wachezaji walioshiriki ligi hiyo, ambao kwa siku za hivi karibuni wamechaguliwa kwenye kikosi kipya cha timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys).

12: Inawakilisha idadi ya wachezaji wanaofuatiliwa kwa karibu na Azam FC baada ya kuonyesha viwango vizuri kwenye michuano hiyo.

30: Hayo ni jumla ya mabao yaliyofungwa na timu iliyofunga mabao mengi kwenye michuano hiyo, ambayo ni mabingwa JMK Park.

11: Hii inamuhusu mshambuliaji wa JMK Park, Flavian Ngonyani, ambaye ameibuka mfungaji bora wa michuano hiyo kwa kufunga idadi hiyo ya mabao.

7: Hii inakwenda kwa kipa bora wa michuano hiyo, Mohamed Yahaya kutoka Azam FC, aliyemaliza michuano hiyo kwa kutoruhusu mabao (cleansheet) katika mechi saba huku akifungwa mabao machache (matano).

8: Ni idadi ya pasi za mwisho alizotoa Rabbin Katuri wa Bom Bom, akiwa ndio mchezaji aliyeandika rekodi ya kutoa pasi nyingi zilizozaa mabao.