KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kucheza dhidi ya Mvuvumwa ya mkoani Kigoma katika mchezo wa kirafiki unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumatano saa 1.00 usiku.

Mchezo huo ni wa pili wa kirafiki kwa Azam FC katika kipindi hiki ligi iliposimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya, baada ya Jumamosi iliyopita kukipiga na Friends Ranger na kutoka sare ya bao 1-1, bao la matajiri hao likifungwa na mshambuliaji mpya Bernard Arthur.

Wakati Azam FC ikiutumia mchezo huo kujinoa kuelekea mechi zijazo, Mvuvumwa itakuwa kwenye maandalizi kuelekea raundi ya pili ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL).

Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Mromania, Aristica Cioaba, limepanga kucheza mechi nne kali za kirafiki katika kipindi hiki cha mapumziko ya ligi, ambapo tayari imeshacheza mechi moja tu wikiendi iliyopita.

Mechi hizo ni sehemu pia ya mazoezi ya kumuunganisha kwenye timu na wachezaji wenzake, mshambuliaji Arthur aliyesajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo akitokea Liberty Professional ya Ghana.

Mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii msimu uliopita wanaodhaminiwa na Maji safi kabisa ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB ambayo ni bora kwa sasa nchini na Tradegents, wamekuwa na mwenendo mzuri kwenye ligi baada ya kucheza mechi 11 na kujikusanyia jumla ya pointi 23.

Katika mechi hizo imeshinda mechi sita na sare tano ikiwa kwenye nafasi ya pili sawa na kinara Simba waliojikusanyia nao pointi hizo lakini wakiwa juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku ikiwa ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache ikifungwa matatu tu hadi sasa.