MICHUANO ya Ligi ya Vijana ya Azam chini ya umri wa miaka 15 (Azam Youth League U-15) imemalizika usiku huu ikishuhudiwa JMK Park ikiibuka mabingwa na Azam FC ikishika nafasi ya pili.

Ligi hiyo iliyochukua wiki 10 ilikuwa na msisimko mkubwa, ambapo matokeo ya mechi za leo JMK Park iliichapa Rendis bao 1-0 kabla ya Tanzanite kuinyuka Millenium 3-1 na wenyeji Azam FC walioonyesha kandanda safi wakitoka suluhu na Bom Bom.

Ushindi huo wa mabingwa JMK umeifanya kumaliza ligi hiyo ikiwa kileleni kwa pointi 27 wakifuatiwa na Azam waliojizolea 18, Rendis imejikusanyia 16 katika nafasi ya tatu, Bom Bom ya nne ikiwa nazo 11, Tanzanite yenyewe imemaliza na pointi tisa kwenye nafasi ya tano huku Millenium ikifunga mkia kwa pointi zake tatu.