KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imejiwekea malengo ya kufika fainali ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) ikiwemo kulitwaa taji hilo msimu huu.

Kauli hiyo ameitoa Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Idd Nassor Cheche, wakati akizungumzia droo ya michuano hiyo iliyotolewa juzi ikishuhudiwa wakipangwa kuanza na Area C United ya Dodoma, amedai kuwa wameipokea vizuri ratiba hiyo na watajipanga kufanya kweli.

“Sisi malengo yetu ni kufika fainali na tuchukue kombe, kwa hiyo kila mtu tutakayepangiwa naye tunajidhatiti, tunajiandaa vizuri ili tuhakikishe ile dhamira yetu inafikia malengo,” alisema Cheche.

Kocha huyo wa muda mrefu ndani ya Azam FC akianzia majukumu ya kuwa Kocha Mkuu kwenye timu ya vijana (Azam U-20) kabla ya kuteuliwa kuwa Kocha Msaidizi Desemba mwaka jana akiwa chini ya Mromania Aristica Cioaba, alisema kuwa wamejipanga vema msimu huu tofauti na mwaka jana.

“Mwaka huu tumejipanga vizuri zaidi tofauti na mwaka jana na tunaari na wachezaji wanaari na tumepata muda kama hivi wa mazoezi tunafanyia kazi matatizo yetu nafikiri mashabiki waje kwa wingi watusapoti na sisi tutawaonyesha kile ambacho wanastahili kuonyeshwa,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, msimu uliopita iliishia nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kupoteza dhidi ya Simba kwa bao 1-0, mchezo ambao timu hiyo ilicheza pungufu kwa takribani dakika 75 kufuatia kiungo wake Salum Abubakar ‘Sure Boy, kuonyeshwa kadi nyekundu iliyolalamikiwa kuwa na utata.

Mchezo huo dhidi ya Area C United, umepangwa kufanyika Uwanja wa Azam Complex kati ya Desemba 20 na 25 mwaka huu.