KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki ndani ya siku nane zijazo hadi Desemba 13 mwaka huu.

Azam FC itaanza kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki Jumamosi hii dhidi ya Friends Rangers utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku kabla ya kukipiga na Mvuvumwa Desemba 13, zote zikiwa ni timu za Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL).

Mechi hizo ni mahususi kabisa kwa ajili ya kukiweka kwenye ushindani kikosi hicho wakati huu wa mapumziko ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) iliyosimama kwa wiki tatu kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya.

Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Mromania, Aristica Cioaba, limepanga kucheza mechi nne kali za kirafiki katika kipindi hiki cha mapumziko ya ligi ili kuwasaidia wachezaji kuendelea na viwango vyao bora walivyokuwa navyo kwenye ligi.

Aidha mechi hizo pia zitatumika kumuunganisha kwenye timu mshambuliaji mpya wa kikosi hicho, Bernard Arthur, aliyesajiliwa katika usajili huu wa dirisha dogo kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Liberty Professional ya Ghana.

Mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii msimu uliopita wanaodhaminiwa na Maji safi kabisa ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB ambayo ni bora kwa sasa nchini na Tradegents, wamekuwa na mwenendo mzuri kwenye ligi baada ya kucheza mechi 11 na kujikusanyia jumla ya pointi 23.

Katika mechi hizo imeshinda mechi sita na sare tano ikiwa kwenye nafasi ya pili sawa na kinara Simba waliojikusanyia nao pointi hizo lakini wakiwa juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku ikiwa ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache ikifungwa matatu tu hadi sasa.