KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itaanza kutetea taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kumenyana na Jamhuri, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar Januari 2 mwakani saa 10.15 jioni.

Azam FC ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo baada ya kuichapa Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika Januari 13 mwaka huu, lililowekwa kimiani kwa mkwaju mkali wa mbali na Nahodha Himid Mao ‘Ninja’.

Ubingwa huo iliutwaa kwa rekodi ya aina yake ya kutofungwa mchezo wowote wala kuruhusu nyavu zake kutikiswa katika mechi tano ilozocheza za michuano hiyo.

Ratiba ya michuano hiyo iliyotoka siku chache zilizopita, inaonyesha kuwa Azam FC imepangwa Kundi A sambamba na timu nyingine nne ambazo ni Jamhuri (Pemba), Taifa Jang’ombe, Simba na URA ya Uganda ambayo ndio timu pekee iliyoalikwa kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.

Hii ni mara ya pili mwaka huu kwa Azam FC kucheza na Jamhuri, kwenye michuano ya mwaka huu timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na Maji Safi ya Uhai Drinking water, itakumbushia nusu fainali ya mwaka huu kwa kukipiga na Taifa ya Jang’ombe katika mchezo wa pili utakaofanyika Januari 4 saa 10.15 jioni.

Kwenye mchezo wa nusu fainali zilizpokutana timu hizo mwaka huu, Azam FC iliibuka kidedea kwa kuichapa Taifa bao 1-0 lililofungwa kwa shuti la mbali na kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’.

Kama ilivyokuwa kwenye fainali ya mwaka huu, Azam FC itashuka tena dimbani Januari 6 saa 2.15 usiku na kukipiga dhidi ya Simba kabla ya kumalizia mchezo wa mwisho wa Kundi A kwa kumenyana na URA Januari 8 saa 10.15 jioni.

Washindi wawili watakaoongoza kila kundi, wanatarajia kufuzu kwa hatua ya nusu fainali itakayopigwa Januari 10 kabla ya mchezo wa fainali kufanyika Januari 13 saa 2.15 usiku.

Kundi B linaundwa na timu zingine tano, ambazo ni Yanga, Zimamoto, Shaba, Mlandege na JKU.

Azam FC kihistoria imeweza kutwaa ubingwa huo mara tatu, mwaka 2011, 2012 na mwaka huu, ambapo mwakani itaingia kwenye michuano hiyo kusaka taji la nne.