NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Azam FC (NMB Player Of The Month) mwezi Oktoba-Novemba.

Mao aliyeshindanishwa na wachezaji wengine wanne wa Azam FC, akiwemo Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, kipa Razak Abalora na beki Bruce Kangwa, anakuwa mchezaji wa tatu msimu huu kutwaa tuzo hiyo baada ya Yakubu Mohammed kufanya hivyo Agosti-Septemba na mshambuliaji Mbaraka Yusuph aliyeibeba Septemba-Oktoba.

Nahodha huyo msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ametwaa tuzo hiyo baada ya kujizolea kura 320 za mashabiki zikiwa ni asilimia 47 ya kura zote 680 zilizopigwa kupitia mtandao wa poll kwenye akaunti ya facebook ya Azam FC.

Aidha kipa mahiri wa timu hiyo, Razak Abalora, ambaye mpaka sasa amefungwa mabao matatu kwenye mechi 11 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ameshika nafasi ya pili baada ya kujizolea kura 292 sawa na asilimia 43 za kura zote zilizopigwa.

Beki wa kushoto, Kangwa ameshika nafasi ya nne kwa kura 41 alizojizolea (asilimia sita) huku Moris akimalizia orodha hiyo baada ya kukusanya kura 27 zikiwa ni asilimia nne za kura zote zilizopigwa na mashabiki (680).

Tuzo hiyo inadhaminiwa na Wadhamini wakuu wa Azam FC, Benki ya NMB, ambayo kwa sasa ndio bora kabisa Tanzania ikikuhakikishia usalama wa fedha zako na ikiwa na matawi mengi yaliyosambaa kote hapa nchini.

#CongratsHimidMao