KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka sare ya baoa 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam usiku huu.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 23 kwenye msimamo wa ligi hiyo sawa na vinara Simba wanaoongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake ilishuhudiwa timu zote zikionyeshana upinzani lakini Azam FC ilionekana kuutawala kwa kiasi fulani, ambayo ilijipatia bao la uongozi dakika ya 56 likifungwa kwa kichwa na winga Enock Atta akiunganisha krosi iliyopigwa na Mbaraka Yusuph.

Hilo ni bao la kwanza kwa Atta kwenye msimu huu wa ligi likiwa pia la kwanza kufunga katika ligi hiyo tokea usajili wake ulipokamilika msimu huu.

Mtibwa Sugar ilisubiri hadi dakika ya 75 kuweza kusawazisha bao hilo lililofungwa na mshambuliaji Kelvin Sabato kwa mpira wa adhabu ndogo ya moja kwa moja nje kidogo ya eneo la 18.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alianza kutumikia adhabu yake ya kutokaa benchini kwa mechi tatu kuanzia mechi ya leo (Mtibwa Sugar) baada ya Kamati ya Saa 72 kudai alimzonga mwamuzi kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting.

Mara baada ya mchezo huo, ligi hiyo inatarajia kusimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika nchini Kenya kuanzia mwezi ujao huku timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ikiwa ni moja ya timu shiriki.

Kutokana na programu hiyo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku tatu na kuanza rasmi mazoezi Ijumaa hii kuendelea na maandalizi ya mechi zijazo. 

Kikosi cha Azam leo:

Razak Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Salmin Hoza, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 83, Frank Domayo/Idd Kipagwile dk 64, Yahya Zayd, Salum Abubakar, Mbaraka Yusuph