KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo imepokea ugeni kutoka Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) waliokuja kutembelea mandhari ya viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mmoja wa maofisa wa Fufa waliofika Azam Complex ni Mtendaji Mkuu Msaidizi wa shirikisho hilo, Humphrey Mandu, ambaye pia ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Ligi Kuu Uganda inayodhaminiwa na Kampuni ya Azam Media kupitia Azam TV (Azam Uganda Premier League).

Mbali na kutembelea Azam Complex, ugeni huo kutoka nchini Uganda umekuja nchini kwa ziara maalumu ya kuwatembelea wadhamini wa ligi yao Azam TV na kampuni za Azam kiujumla na kuangalia namna walivyofanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Meneja wa Uwanja wa Azam FC, Sikitu Salim, ndiye aliyepokea ugeni huo na kuwatembeza maeneo mbalimbali wageni hao ndani ya Azam Complex, kama vile uwanja, gym, Media Center na vyumba wanavyolala wachezaji.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mandu alisifia uwekezaji uliofanywa ndani ya Azam FC akidai kuwa ni wa kushangaza sana na kiwango cha hali juu.

“Azam Complex ni moja ya kituo ambacho ni bora, tunafuraha na Azam kwa inachokifanya Uganda ni kitu cha kushangaza ikidhamini ligi (Azam Uganda Premier League) wakiwa wadhamini wakuu wa ligi, hivi sasa tulivyotembelea Azam Complex hapa Dar es Salaam imetupa matumaini mazuri kuwa Azam ni taasisi inayothamini soka na inaweza kuendeleza.

“Hiyo inamaanisha kuwa tunafanya kazi na taasisi sahihi katika kusaidia maendeleo ya soka Uganda, tukiwa kama watu wa mpira tunafuraha kuona kuwa Azam imewekeza ipasavyo kwenye soka la Uganda na Tanzania, tumeona uwanja mkubwa mzuri na wa ajabu, nimewahi kufanya ukaguzi wa viwanja hapa Afrika lakini huu uwanja (Azam Complex) ni moja ya viwanja bora,” alisema.

Alisema Azam FC ni moja ya klabu nzuri huku akiitabiria makubwa ya kuwa na jina kubwa hapo baadaye kutokana na uwekezaji uliofanywa na namna inavyoendeshwa akidai itakuwa timu kubwa Afrika.

“Kwa sasa imeshakuwa kubwa hapa Afrika Mashariki na Tanzania, imetupa somo kubwa kwenye ukanda huu kwa mfano ni vizuri kwa klabu kuwa na uwanja wake inaomiliki, inasaidia kujiamini miongoni mwa wachezaji hii kwa sababu wachezaji wanajua wapo nyumbani kitu ambacho kinaipa faida klabu kwenye mechi dhidi timu inayotembelea (timu pinzani),” alisema.

Mandu alimalizia kwa kusifia namna mfumo wa utendaji kazi ulivyopangiliwa pamoja na miundombinu mingine ndani ya Azam Complex akisema kuwa vitu hivyo ndivyo vinavyotakiwa Afrika kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya soka hususani Afrika Mashariki.

“Napenda kuishukuru Azam, Azam Group of Company, asante kwa Abubakar (Bakhresa) na timu yake hapa Dar es Salaam mnafanya kazi nzuri sana ya kuendeleza soka la ukanda huu (Afrika Mashariki),” alisema.