KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendeleza wimbi la ushindi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Njombe Mji bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Sabasaba, mkoani Njombe jioni ya leo.

Alikuwa ni Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Agrey Moris aliyekuwa nahodha wa mchezo wa leo, akiihakikishia ushindi timu hiyo kwa bao safi la mkwaju wa penalti dakika ya 60 baada ya Enock Atta kufanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari.

Hilo ni bao la kwanza la Moris msimu huu.

Huo ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Azam FC, ikifikisha jumla ya pointi 22 kwenye msimamo wa ligi hiyo katika nafasi ya pili ikiwa sawa na kinara Simba, ambayo inaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mbali na kuwa sehemu nzuri kwenye msimamo wa ligi, pia kipa wa Azam FC, Razak Abalora, amezidi kuonyesha ubora wake baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi ya nane ya ligi kati ya 10, bila kufungwa bao lolote huku akiruhusu nyavu zake kuguswa mara mbili tu.

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo, ikiwakosa nyota wake watatu wa kikosi cha kwanza waliokuwa na kadi tatu za njano, ambao ni Nahodha Himid Mao ‘Ninja’ na mabeki Yakubu Mohammed, Daniel Amoah huku pia ikiwakosa wengine wawili viungo Braison Raphael na Masoud Abdallah ambao ni majeruhi.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, aliziba mapengo yao kwa kuwanzisha kikosini mabeki David Mwantika, Swaleh Abdallah aliyebadilishana na Abdallah Kheri dakika ya 46, na kiungo Salmin Hoza, ambaye alicheza nafasi ya Himid.

Aidha katika mchezo huo uliokuwa wa ushindani mkubwa na mgumu kwa pande zote mbili, ilishuhudia Azam FC ikitengeneza nafasi ya kwanza dakika ya sita kwa kufanya shambulio zuri lakini shuti alilopiga Mbaraka Yusuph lilitoka nje ya lango.

Atta aliyeendelea kuwa kwenye kiwango kizuri, alionekana kuipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya Njombe Mji muda wote wa mchezo huo kabla ya kutolewa dakika ya 89 na kuingia kiungo mkabaji Stephan Kingue.

Azam FC ilipata pigo dakika ya 74 baada ya kuumia kwa mshambuliaji wake Mbaraka Yusuph, ambaye alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Idd Kipagwile.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu alfajiri, tayari kabisa kuanza maandalizi ya kukabiliana na Mtibwa Sugar, mchezo unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex Novemba 27 saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Swaleh Abdallah/Abdallah Kheri dk 46, Bruce Kangwa, David Mwantika, Agrey Moris (C), Salmin Hoza, Enock Atta/Stephan Kingue dk 89, Frank Domayo, Yahya Zayd, Salum Abubakar, Mbaraka Yusuph/Idd Kipagwile dk 74