NAHODHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Agrey Moris, amewaambia mashabiki wa timu hiyo watarajie mambo mazuri kuelekea mchezo wa keshokutwa Jumapili dhidi ya Njombe Mji.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) unatarajia kufanyika Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe, ambapo Azam FC leo imemaliza mazoezi ya pili tokea iwasili mkoani humo tayari kabisa kufanya maandalizi ya mwisho.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Moris alisema kuwa wanajua mchezo huo utakuwa sio rahisi lakini kwa maandalizi mazuri waliyopata wamejipanga kufanya vizuri.

“Mashabiki watarajie mambo mazuri kwa sababu kama timu tumejiandaa vizuri, tunajua mchezo utakuwa si rahisi ila kama sisi wachezaji tumejipanga kuhakikisha kila mchezo uliokuwa mbele tunapata pointi tatu,” alisema.

Akizungumzia kukosekana kwa baadhi ya wachezaji kuelekea mchezo huo kama vile nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Daniel Amoah na Yakubu Mohammed, alisema hiyo ni nafasi kwa wachezaji wengine watakaopata nafasi kuweza kumshawishi kocha na timu kupata matokeo mazuri.

“Mimi naweza kusema wale ni wachezaji muhimu ila ukiangalia timu ina wachezaji wengi na wote wachezaji muhimu kwa hiyo hii ni nafasi kwa wachezaji wengine ambao hawakupata nafasi kuhakikisha wanaonyesha uwezo wao kumshawishi mwalimu kuhakikisha tunapata matokeo,” alimalizia mchezaji huyo mkongwe ndani ya kikosi cha Azam FC.

Hadi sasa ligi ikiwa inaelekea raundi ya 10, Azam FC ipo nafasi ya pili baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 19 sawa na Simba iliyokileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku ikiwa ndio timu pekee iliofungwa mabao machache hadi sasa ikiruhusu mawili tu.