KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kipo mguu sawa kuelekea mkoani Njombe kucheza na wenyeji wao Njombe Mji, kikitarajia kuanza safari keshokutwa Jumatano Alfajiri.

Azam FC ipo kamili kabisa kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Sabasaba Jumamosi hii, ambapo kikosi hicho kinaendelea na mazoezi makali kwenye viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita wamekuwa na rekodi nzuri tokea msimu huu ulipoanza, ambapo katika mechi tisa za ligi walizocheza hawajapoteza mchezo wowote, wakishinda tano na kutoka sare mara nne huku ikiwa ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache, ikifungwa mawili tu.

Ubora wake huo umeifanya kujikusanyia jumla ya pointi 19 katika nafasi ya pili kwenye msimamo sawa na Simba iliyo kileleni wka tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kikosi hicho kipo kamili kabisa licha ya kwenye mchezo ujao kuwakosa wachezaji wake watatu wenye kadi tatu za njano, ambao ni mabeki Yakubu Mohammed, Daniel Amoah na nahodha Himid Mao ‘Ninja’.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, tayari ameshaweka wazi kuwa amelenga kuendeleza wimbi la ushindi kwenye mchezo ujao, huku akiwaomba wachezaji kuendeleza hali ya kupambana walioonyesha katika mechi zilizopita.

“Kila mechi ni tofauti, umakini tumeuweka kwa wapinzani wetu hivi sasa tunawiki mbili za maandalizi ya mchezo ujao (Njombe Mji), sio rahisi kucheza ugenini hapa Tanzania, ni ngumu lakini napenda kwenda na kukusanya pointi tatu.

“Haitakuwa rahisi lakini wachezaji wanatakiwa kuelewa kama unafanya kazi bidii kila mmoja ataheshimu jina lako, kila mmoja atamuheshimu mpinzani, inawezakana ukashinda mchezo,” alisema Ciaoba wakati akianza maandalizi kuelekea mchezo huo wiki iliyopita.

Jumamosi iliyopita Azam FC iliwapima wachezaji wake kwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 ‘Kilimanjaro Heroes’, na mabingwa hao wakaibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na Nahodha Msaidizi Agrey Moris na Joseph Mahundi.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Azam FC kukipiga na Njombe Mji katika mechi rasmi ya mashindano, lakini itakumbukwa kabla ya kuanza msimu huu timu hizo zilicheza mchezo wa kirafiki wakati wa maandalizi na Njombe kushinda mabao 2-0.