WIKI ya tano ya Ligi ya Vijana ya Azam chini ya umri wa miaka 15 (Azam Youth League U-15) imemalizika mchana huu kwa timu za Azam FC, JMK Park na Rendis kufanya kweli.

Mchezo wa kwanza ilishuhudiwa JMK Park ikiendeleza wimbi la ushindi kwenye michuano hiyo baada ya kuichapa Rendis mabao 2-1.

Wenyeji Azam FC walipata ushindi wa chee wa mabao 3-0 dhidi ya Bom Bom, kufuatia timu hiyo kushindwa kukamilisha taratibu za mashindano hayo za kulipia ada ya ushiriki ambayo mwisho wake ilikuwa wikiendi iliyopita.

Tanzanite nayo ikapata ushindi kama huo wa mezani kufuatia timu mpya ya  Millenium kushindwa kumalizia taratibu za kikanuni za kuwaruhusu kushiriki michuano hiyo.

Michuano hiyo itaendelea tena Novemba 18 mwaka huu, Bom Bom ikimenyana na JMK Park saa 2.30 asubuhi, Tanzanite itafuatia ikichuana na Rendis huku Millenium na Azam FC zikifunga dimba kwenye mchezo wa mwisho.