KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, amewaomba wachezaji wake kuendeleza hali ya kupambana katika mechi zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kikosi cha timu hiyo tayari kinaendelea na mazoezi tokea Jumanne ijayo kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Njombe Mji, utakaofanyika Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe Novemba 18, mwaka huu.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo kwa pointi 19 sawa na Simba, ambayo ipo kileleni kutokana na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Cioaba ameuambia mtandao wa klabu www.azamafc.co.tz tayari wachezaji wameelewa falsafa yake huku akizitaka pande zote ndani ya timu hiyo kushikamana na kuwa na umoja kwenye kipindi hiki ambacho timu hiyo inawania taji la ligi.

“Napenda kuongelea kuhusu wachezaji, ninafuraha kutokana na wachezaji kuelewa falsafa yangu kabla ya ligi kuanza niliongea na kila mmoja, mnaona kila mmoja haiamini timu hii changa, lakini walifanya kazi kubwa kwenye maandalizi ya msimu (pre season), tulienda Uganda tulikutana na timu ngumu na tukawa na programu ngumu, tulirejea na kuendelea na mazoezi magumu kila wiki na wachezaji wakaelewa na sasa tupo juu kwenye ligi.

“Lakini hii haijamalizika katika baadhi ya mechi tumekuwa na baadhi ya matatizo uwanjani, ambapo kila mmoja amekuwa akipenda tufunge mabao mengi kwenye mpira, mashabiki ndio wanataka hivyo lakini wanachotakiwa kuelewa ni sio rahisi kwenye mpira kushinda mechi 1-0, hiki ni kiwango kizuri kwani timu imekuwa ikikaa vizuri kimbinu ndani ya uwanja, kila mmoja anaiamini timu, kila mmoja anaamini kundi hili na kwa sasa timu imekaa juu,” alisema.

Aidha Cioaba aliongeza kuwa: “Naiamini timu hii, kiukweli naiamini timu hii, naliamini benchi langu la ufundi (staff), naiamini kazi yangu na inatakiwa kuendelea kupambana na napenda kuongea na kila mmoja kuhusu jambo moja kuwa wote tufanye kazi kwa umoja.”

Kuelekea mechi na Njombe Mji    

Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Njombe Mji, Cioaba alisema kuwa ana wiki mbili za maandalizi kabla ya kuvaana na timu hiyo huku akitanabaisha ya kuwa kikosi chake kitacheza mchezo mmoja wa kirafiki Jumamosi hii saa 10.00 jioni.

“Kila mechi ni tofauti, umakini tumeuweka kwa wapinzani wetu hivi sasa tunawiki mbili za maandalizi ya mchezo ujao (Njombe Mji), sio rahisi kucheza ugenini hapa Tanzania, ni ngumu lakini napenda kwenda na kukusanya pointi tatu, kutokana na hilo nimeanza na mazoezi ya nguvu wiki hii, kila siku mazoezi ni mara mbili, wachezaji wanafanya kazi kwa bidii na Jumamosi nina mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya timu nzuri, nimeweka umakini mkubwa kwenye mchezo ujao, nataka kurejea na pointi zote tatu.

“Haitakuwa rahisi lakini wachezaji wanatakiwa kuelewa kama unafanya kazi bidii kila mmoja ataheshimu jina lako, kila mmoja atamuheshimu mpinzani, inawezakana ukashinda mchezo,” alimalizia kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana.

Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora kabisa nchini ya NMB na Tradegents, imefikisha jumla ya pointi 19 katika nafasi ya pili baada ya kushinda mechi tano na kutoka sare michezo minne huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.