LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) imemaliza raundi ya tisa wikiendi iliyopita huku ikionekana kufikia patamu kutokana na upinzani mkubwa unaoonyeshwa na timu zote shiriki.

Ukweli wa kauli hiyo umedhihirishwa na matokeo yaliyopatikana kwenye raundi hiyo, ambapo ni timu mbili pekee zilizoweza kuibuka na ushindi huku mechi sita zilizobakia zikiisha kwa sare.

Timu zilizoweza kuibuka na ushindi ni Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, iliyoifunga Ruvu Shooting bao 1-0 na kufikisha jumla ya pointi 19 ikiwa nafasi ya pili sawa na kinara Simba, ambayo nayo iliifunga Mbeya City ushindi kama huo jana.

Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, mpaka sasa ligi ikimaliza raundi ya tisa imeonyesha umwamba baada ya kufanikiwa kushinda jumla ya mechi tano, sare nne na kutopoteza mchezo wowote.

Ukiangalia takwimu za mechi zote hizo tano ilizoshinda, ni mechi mbili tu ambazo Azam FC iliweza kupata bao kipindi cha pili, zingine zilizobakia ilifunga kipindi cha kwanza huku ikiwa na wastani wa kushinda bao moja katika kila ushindi.

Mbali na timu nne za juu kuonyeshana upinzani mkubwa, Simba, Azam FC zenye pointi 19 na Yanga, Mtibwa Sugar zilizofikisha 17 kila mmoja, pia upinzani umeonekana kuwa mkubwa sana kwa timu zinazofuatia, na tofauti ya timu mbili za juu hadi ile inayoshika nafasi ya saba Lipuli kwa pointi 13 imeonekana kuwa ni pointi sita, jambo ambalo linazidi kudhihirisha ushindani wa ligi hiyo.

Ikiwa na safu bora ya ulinzi, hadi sasa ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache baada ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu, ilipocheza na Singida United (1-1) na Mwadui (1-1) mechi zote zikiwa ugenini.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, wamecheza jumla ya mechi tano nyumbani na nne ugenini, na jambo zuri imekuwa ndio timu pekee ambayo haijaruhusu nyavu zake kutikiswa ikicheza nyumbani.

Aidha katika pointi 19 ilizojikusanyia, imepoteza jumla ya pointi nane tu zilizotokana na sare nne ilizopata hadi sasa, moja ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani ilipotoka suluhu na Simba, huku zikingine tatu zikiwa za ugenini dhidi ya Singida United (1-1), Mwadui (1-1) na suluhu dhidi ya Mbao katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Kinara wa ufungaji mabao mpaka sasa kwa Azam FC ni mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyefunga mabao matatu kwenye ligi hiyo, akifuatiwa na wengine waliofunga bao moja kila mmoja, ambao ni nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Yahya Zayd, Paul Peter na Yahaya Mohammed.

Pamoja na kuwa kinara, pia Yusuph amesaidia kupatikana kwa bao moja la Azam FC walipocheza na Mwadui baada ya kuangushwa ndani ya eneo la 18 na kumpa nafasi Himid kuipatia bao kwa njia ya mkwaju wa penalti.

Wengine waliotoa pasi za mabao ni Himid, Zayd, winga Enock Atta na mabeki Bruce Kangwa, Aggrey Moris na Daniel Amoah, wote wakichangia pasi moja kila mmoja zilizozaa mabao.

Baada ya mechi za wikiendi iliyopita, wiki hii ligi hiyo imesimama hadi wiki ijayo kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambapo timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakipiga dhidi ya Benin kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaofanyika nchini humo wikiendi hii.

Wachezaji wa Azam FC walipata mapumziko wa siku mbili baada ya mechi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting, ambapo kesho Jumanne jioni kitaanza rasmi maandalizi ya kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Njombe Mji, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sabasaba, mkoani Njombe Novemba 18 mwaka huu.