MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yahya Zayd, amewaomba mashabiki wa timu hiyo kushusha presha huku akiwaambia mambo mazuri zaidi yanakuja muda si mrefu.

Kauli ya kinda huyo imekuja muda mchache mara baada ya kufunga bao muhimu usiku wa kuamkia leo, lililoihakikishia pointi tatu muhimu Azam FC wakati ikiichapa Ruvu Shooting bao 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Hilo linakuwa ni bao lake la tatu kuifungia Azam FC baada ya kupandishwa akitokea timu ya vijana ya timu hiyo (Azam U-20), na bao lake la kwanza linalomtambulisha kwenye ligi hiyo, mengine mawili akifunga katika mechi za kirafiki za maandalizi ya msimu mpya la kwanza akitupia dhidi ya Lipuli (4-0) na jingine Azam FC ilipoilaza Onduparaka ya Uganda mabao 3-0.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Zayd alisema kuwa ni jambo la faraja kwake kuweza kuifungia bao muhimu timu hiyo huku akisema bao hilo limemfungulia njia ya kufanya vizuri zaidi kuelekea mechi zinazokuja.

“Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuisaidia timu yangu kuibuka na pointi tatu, haikuwa kazi rahisi kupata ushindi huo tumepambana kwa dakika zote na hatimaye mwishoni tukafanikiwa kuibuka na ushindi, hii ni historia kwangu.

“Mashabiki wasikate tamaa waendelee kutuunga mkono na washushe presha kwani mambo mazuri zaidi yanakuja, tunawaomba waje kwa wingi uwanjani kutushangilia hata pale tunapokosea basi waendelee kututia nguvu kwa kutushangilia,” alisema Zayd.

Ushindi huo uliiwezesha Azam FC kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa muda ikifikisha jumla ya pointi 19, kabla ya leo kushuka kwa nafasi moja baada ya Simba kuifunga Mbeya City bao 1-0 nayo ikifikisha pointi 19 lakini inakaa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa..

Lakini hadi sasa timu zote za ligi hiyo zikiwa zimeshacheza mechi tisa, Azam FC imeonekana kuwa na safu kali ya ulinzi kwani inashikilia rekodi ya kufungwa mabao machache, ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.