KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Idd Nassor Cheche, amewaomba mashabiki wa timu hiyo na wapenzi wa soka wajitokeze kwa wingi kesho Jumamosi kushuhudia wanavyofungua ukurasa mpya wa umaliziaji.

Azam FC itashuka kwenye Uwanja wa Azam Complex kesho kuvaana na Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) unaotarajia kufanyika saa 1.00 usiku.

Kwa muda mrefu tokea ligi hiyo ianze Agosti 26 mwaka huu, timu hiyo imekuwa na mwenendo mzuri kabisa lakini ikishindwa kupata ushindi mnono katika mechi nne ilizoshinda huku ikiwa na safu bora ya ulinzi baada ya kuruhusu mabao mawili tu ya kufungwa.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuelekea mchezo huo, Cheche alisema kuwa kikosi chake kimejiandaa vilivyo na wachezaji wanaari kubwa ya kufanya vizuri.

“Tumejiandaa vizuri na wachezaji wote wa ari, tumejiandaa kiakili, kiufiti, kisaikolojia kwa hiyo tunasema mashabiki wetu waje kwa wingi kesho tunataka tufanye jambo,” alisema.

Alipoulizwa wamejipangaje kukabiliana na upinzani kutoka kwa wapinzani wao, Cheche alisema wanafanya maandalizi ya kujiandaa kukabiliana na timu zote na sio timu moja.

“Sisi kwanza tumejiandaa katika michezo yetu yote ya ligi ukiondoa na Ruvu Shooting, halafu timu yetu kwa sababu ni timu ambayo kila timu ikija kucheza na sisi inakuwa inajiandaa vizuri, kwa hiyo na sisi tunajiandaa zaidi yao.

“Na vilevile tunasema uwanja wetu unachezeka kwa mtu anayejiandaa kucheza akifika kwetu kwa sababu uwanja umekaa vizuri atacheza mpira, kwa hiyo katika kulijua hilo na sisi tunajiandaa mara mbili zaidi yao,” alisema.

Huo utakuwa ni mchezo wa 13 kihistoria kwa Azam FC kukutana na Ruvu Shooting kwenye mechi za ligi hiyo, ambapo katika michezo iliyopita Azam FC imeshinda mara saba na mechi tano zilizobakia zikiisha kwa sare.

Rekodi zinaonyesha kuwa katika mechi hizo ambazo Azam FC ilishinda, ni mechi mbili tu zilizoisha kwa mabingwa hao kutoka uwanjani wakiwa wamefunga bao moja, ambapo zingine zote zilizobakia ilipata ushindi wa wastani wa kuanzia mabao mawili hadi manne.

Ikiwa imetoka kuipiga Ashanti United mabao 4-0 kwenye mchezo wa kirafiki juzi, timu hiyo inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora kabisa nchini ya NMB na Tradegents, itaingia dimbani ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 16 katika nafasi ya nne ikiwa sawa na timu tatu zilizokuwa juu yake ambazo ni Simba, Yanga na Mtibwa Sugar.