KOCHA mpya wa timu ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam U-10), Meja mstaafu Abdul Mingange, amekiongoza kikosi hicho kwa mara ya kwanza jana jioni kwa kuichapa Jackys Academy ya Mbagala mabao 2-0.

Mchezo huo wa kirafiki ulifanyika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, ambapo Mingange amekabidhiwa kuinoa timu hiyo akirithi mikoba ya Idd Nassor Cheche, ambaye kwa sasa ni Kocha Msaidizi wa Azam FC chini ya Mromania, Aristica Cioaba.

Kikosi hicho kilionekana kucheza vema katika kila kipindi, lakini kitajilaumu baada ya kupoteza nafasi za kufunga mabao kipindi cha kwanza kabla ya kujipatia mabao yaliyoipa ushindi kipindi cha pili.

Muuaji wa Jackys Academy inayomilikiwa na Jamal Kisongo, ambaye ni Meneja wa staa wa Tanzania anayecheza Genk ya Ubelgiji Mbwana Samatta, alikuwa ni mshambuliaji Hutham Saadun, aliyefunga mabao yote mawili dakika ya 63 na 81 akimalizia kazi nzuri zilizofanywa na Maulid Tamila na Abdallah Mkulu.

Azam U-20 imekuwa ikicheza mechi kadhaa za kirafiki kila wiki ili kujiweka sawa kimchezo kutokana kuwa na uhaba wa michuano ya vijana nchini, ambapo baadaye mwaka huu inatarajia kushiriki Ligi ya Vijana kwa timu za vijana za umri huo zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).