KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, usiku huu imeichapa Ashanti United mabao 4-0, katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Mchezo huo ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya kuwaweka kwenye ushindani wachezaji, pia wakipasha misuli kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ruvu Shooting utakaofanyika uwanja huo Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

Azam FC ilifanikiwa kutawala vipindi vyote vya mchezo huo, huku benchi la ufundi likichezesha vikosi viwili tofauti katika kila kipindi cha mchezo huo, isipokuwa wachezaji wawili beki wa kulia, Swaleh Abdallah na kiungo Masoud Abdallah, ambao ni majeruhi.

Mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii msimu uliopita walijipatia mabao mawili katika kila kipindi, ambapo winga Enock Atta, aliyeendelea kuwa kwenye kiwango chake kizuri alifunga bao la uongozi dakika ya nane baada ya kuitoka safu ya ulinzi ya Ashanti na kupiga shuti lililojaa wavuni.

Winga Idd Kipagwile, alipigilia msumari wa pili dakika ya 31 baada ya kuingia kwa kasi kwenye eneo la 18 la Ashanti na kupiga shuti lililomshinda kipa na hivyo kufanya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika kwa uongozi wa mabao mawili ya Azam FC huku Ashanti wakiwa hawajapata kitu.

Kipindi cha pili Azam FC ilihitimisha ushindi huo mnono kwa mabao mengine mawili, yaliyofungwa na mshambuliaji Wazir Junior dakika ya 75 na jingine likiwekwa kimiani kwa mkwaju wa penalti na beki David Mwantika dakika ya 86.

Kiungo Salmin Hoza, angeweza kuipatia mabao mengine mawili Azam FC baada ya mashuti yake mawili aliyopiga kugonga mwamba.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kimeingia moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting, utakaofanyika wikiendi hii.

Kikosi cha Azam FC

Razak Abalora/Mwadini Ally dk 46, Daniel Amoah/Joseph Mahundi dk 46, Bruce Kangwa/Braison Raphael dk 46, Aggrey Moris/David Mwantika dk 46, Yakubu Mohammed/Abdallah Kheri dk 46, Himid Mao (C)/Stephan Kingue dk 46, Salum Abubakar/Salmin Hoza dk 46, Idd Kipagwile/Frank Domayo dk 46, Mbaraka Yusuph/Yahaya Mohammed dk 46/Kangwa dk 72, Yahya Zayd/Wazir Junior dk 46, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 46