KOCHA mpya wa timu ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam U-20), Meja Mstaafu Abdul Mingange, ameweka wazi kuwa moja ya mikakati yake ni kuifanya timu hiyo kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali pamoja na kupandisha wachezaji watakaoongeza nguvu katika timu kubwa.

Kocha huyo wa zamani wa baadhi ya timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kama vile Ndanda na Tanzania Prisons, jana alitangazwa rasmi kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho akichukua mikoba ya kocha wa muda mrefu wa timu hiyo, Idd Nassor Cheche, ambaye kwa sasa ni Kocha Msaidizi wa Azam FC tokea mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana.

Akifanya mahojiano na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Mingange alisema kuwa kwa muda wa mwezi mmoja hadi miwili ijayo, timu hiyo itakuwa na mtazamo tofauti chini yake tofauti na ilivyo sasa huku akiweka wazi kushirikiana na watangulizi wake waliokuwa wakikinoa kikosi hicho.

“Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata bahati ya kuja kuwepo kwenye timu ya Azam FC hasa kwenye timu ya vijana kwa sababu mimi napenda sana kufundisha vijana na nilishafanya hivyo miaka iliyopita, kwa hiyo kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hiyo kwa kujumuika katika klabu kubwa kama hii yenye kila kitu katika mpira wa Tanzania.

“Lakini vilevile nafikiri uongozi wameona juhudi zangu katika sehemu hizo nilizopita na wameona sifa nilizonazo naweza kidogo nikaongeza jambo hapa kwenye timu yetu kwa hilo tu nasema na mimi nitajitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuhakikisha timu yetu ya vijana infanya vizuri na tunaweza kupandisha vijana wakeongeza nguvu kwenye timu yetu kubwa,” alisema Mingange.

Kujua alichoongea zaidi, bofya kwenye link hii ya chaneli yetu ya YouTube: https://youtu.be/j1lSUr5aLPg