KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeanza rasmi mazoezi leo asubuhi tayari kabisa kuiwinda Ruvu Shooting.

Azam FC  itakipiga na maafande hao katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi, wameanza maandalizi wakiwa na kikosi chote kamili, akiwemo beki wa kulia Swaleh Abdallah, aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu ya mguu wakati Azam FC ikijiandaa kukabiliana na Mbao wiki moja iliyopita.

Kikosi hicho kitaendelea tena na mazoezi kesho Jumanne kwa mazoezi mara mbili kabla ya kucheza mchezo mmoja wa kirafiki wa kupasha misuli joto na wachezaji kuingia moja kwa moja kambini kwenye viunga vya Azam Complex, tayari kabisa kufanya maandalizi ya mwisho ya mtanange huo.

Timu hiyo inayodhaminiwa na maji safi kabisa ya Uhai Drinking Water, Benki bora kabisa nchini ya NMB na Tradegents, imekuwa na msimu mzuri hadi sasa ikiwa haijapoteza mchezo wowote kwenye mechi nane za ligi ilizocheza mpaka sasa, ikiwa imeshinda nne na kutoka sare nne.

Azam FC ni miongoni mwa timu tano za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo zinazofukuzia ubingwa msimu huu ikijikusanyia pointi 16, ikiwa inalingana pointi na timu nyingine tatu zilizo juu yake kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ambazo ni Simba, Yanga na Mtibwa Sugar.

Jambo la kufurahisha zaidi linaloifanya kuwa na rekodi nzuri, ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache mpaka sasa ikiwa imeruhusu nyavu zake kuguswa mara mbili na katika mechi nane ilizocheza, imefanikiwa kutoka uwanjani bila wavu wake kuguswa kwenye mechi sita.

Mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyeibuka kinara Mchezaji Bora wa Azam FC wa mwezi Septemba-Oktoba (NMB Player of the Month) ndiye anayeongoza mpaka sasa kwenye kucheka na nyavu ndani ya kikosi hicho akiwa ametingisha nyavu za wapinzani mara tatu.