LICHA ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City usiku wa kuamkia leo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, amedai kuwa haikuwa mechi nyepesi kutokana na upinzani mkubwa ulioonyeshwa na wapinzani wao.

Bao pekee lililoipa Azam FC pointi tatu, lilifungwa na Mchezaji Bora wa Azam FC (NMB Player of the Month) mwezi Septemba-Oktoba, mshambuliaji Mbaraka Yusuph, akitumia vema kona iliyochongwa na winga Enock Atta na mpira kumgonga mgongoni baada ya kumponyoka kipa wa Mbeya City, Owen Chaima.

Cheche ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho huku akidokeza kwamba kama mechi zote za ligi zingekuwa zikichezwa kwa kiwango hicho basi soka la Tanzania lingepiga hatua.

“Nafurahi kwa ushindi na vile vile nafurahi kwa kiwango na ushindani tuliokutana nao katika mechi, kama tunakuwa tunacheza ligi katika mechi zote kwa namna hii nafikiri kiwango chetu cha mpira Tanzania kingekwenda juu, lakini inatokezea baadhi ya mechi moja moja mechi nyingi zinakuwa na matatizo,” alisema.

Ukitaka kujua alichoongea zaidi bofya hapa: https://youtu.be/vYzMoadkqWo