KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, usiku huu imeichapa Mbeya City bao 1-0, ushindi ulioifanya ikamate usukani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC imepanda kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 16 ikizizidi pointi moja Simba, Yanga na Mtibwa Sugar zenye pointi sawa zote zikiwa na 15, ambazo zinatarajia kucheza kesho Jumamosi kwenye mechi zake za raundi ya nane.

Bao pekee la Azam FC limefungwa na mshambuliaji Mbaraka Yusuph, akimalizia mpira wa kona uliochongwa na Enock Atta Agyei.

Azam FC ilianza vema mchezo huo, ambapo katika dakika ya kwanza mpira wa krosi uliochongwa na Atta ulikosa mmaliziaji na kudakwa kiurahisi na kipa wa Mbeya City, Owen Chaima.

Dakika ya nane beki Daniel Amoah, alifanya shambulizi kali langoni mwa Mbeya City baada ya kupanda kwa haraka lakini pande alilopiga linashindwa kumaliziwa vema na Yahya Zayd, aliyepiga shuti lililotoka nje ya lango.

Winga Enock Atta, aliyekuwa kwenye kiwango vizuri alipiga mpira mzuri wa faulo dakika ya 19 uliokuwa ukielekea nyavuni lakini kipa wa Mbeya City alifanya kazi ya ziada baada ya kuupangua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, timu zote zilishindwa kutambiana, ambapo kipindi cha pili Azam FC iliingia na kasi kubwa ikitaka kupata bao la uongozi lakini safu ya ulinzi ya Mbeya City iliweza kuondoa hatari zote.

Alikuwa ni Yusuph dakika ya 59, aliyeweza kuutumia vema uzembe wa kipa wa Mbeya City, Chaima baada ya mpira alioudaka kumtoka kufuatia kona safi iliyochongwa na Atta.

Hilo ni bao lake la tatu kwenye msimu huu wa ligi, mengine mawili akifunga dhidi ya Lipuli (1-0), Kagera Sugar (1-0).

Azam FC iliweza kulinda bao lake hilo, licha ya mashambulizi kadhaa ya Mbeya City kuelekea dakika za mwisho za mchezo huo, ambapo kipa Razak Abalora na safu yake ya ulinzi waliweza kusimama vema.

Baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku mbili hadi Jumatatu asubuhi kitakapoanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Ruvu Shooting utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Tuzo zatoka

Kabla ya kuanza mchezo huo, tuzo ziligawiwa kwa wachezaji bora wa Azam FC mwezi Septemba (timu kubwa na ndogo), Mbaraka Yusuph alikabidhiwa tuzo yake (NMB Player of the Month) na mshambuliaji Paul Peter akibeba ile ya timu ndogo (Uhai Player of the Month).

Kikosi cha Azam FC leo

Razak Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Himid Mao (C), Braison Raphael, Salum Abubakar/Idd Kipagwile dk 69, Mbaraka Yusuph/Frank Domayo dk 85, Yahya Zayd/Yahaya Mohammed dk 73, Enock Atta