KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa kibaruani Ijumaa hii kuvaana na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.

Huo utakuwa ni mchezo wa kwanza wa Azam FC nyumbani mwezi huu baada ya kutoka kucheza mechi tatu mfululizo ugenini, ikifanikiwa kuzoa pointi tatu pekee baada ya sare dhidi ya Singida United (1-1), Mwadui (1-1) na Mbao (0-0).

Tayari kikosi cha Azam FC kimeingia kambini moja kwa moja jana tokea kilipotoka kucheza na Mbao mkoani Mwanza, ikiwa ni mikakati ya kuhakikisha inazoa pointi zote tatu na kuendelea na kasi ya kufukuzia ubingwa wa ligi hiyo.

Baada ya safari ndefu ya kanda ya ziwa, kikosi hicho kinatarajia kuanza rasmi maandalizi ya mchezo huo leo Jumanne, ambapo Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, amesema kuwa wanauchukulia kwa uzito mkubwa mtanange huo wakiwa na lengo la kuibuka kidedea.

Kocha huyo raia wa Romania, amezidi kuwaomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwapa moyo na sapoti wachezaji vijana waliomo kwenye kikosi hicho wakiwemo wale wanaounda safu ya ushambuliaji Yahya Zayd na Mbaraka Yusuph.

Hadi sasa ikiwa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo kwa pointi zake 13 ikizidiwa pointi mbili na Simba, Yanga na Mtibwa Sugar zilizo juu, Azam FC ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache, ikiwa imeruhusu wavu wake kuguswa mara mbili tu.

Mbeya City iliyoshinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza mbili, imejikusanyia pointi 11 ikiwa nafasi ya sita kwenye msimamo.

Rekodi yaibeba Azam FC

Ukiondoa rekodi nzuri ya kuifunga Mbeya City, Azam FC imeonekana kuwa na rekodi nzuri ya kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani tokea msimu huu uanze, ambapo katika mechi tatu ilizocheza imevuna pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na kutoa sare moja dhidi ya Simba (0-0).

Mbeya City yenyewe haijafanikiwa kupata ushindi wowote ugenini msimu huu katika mechi tatu walizocheza, imefanikiwa kupoteza mmoja dhidi ya Stand United (2-1) na kutoka sare mbili walipokipiga na Mwadui (2-2) na Mbao (2-2).

Kihistoria, Azam FC imekutana mara nane na Mbeya City kwenye mechi za ligi hiyo tokea timu hiyo ya jijini Mbeya ilivyopanda daraja mwaka 2013, Azam FC ikiwa imeshinda asilimia 90 za mechi zote ikiibuka kidedea mara nne, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja.

Mchezo ilioupoteza ilitokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipoka pointi tatu Azam FC baada ya kushinda mabao 3-0, ikidai ilimchezesha beki Erasto Nyoni kimakosa kutokana na mchezaji huyo kukusanya kadi tatu za njano.

Vita ya kileleni

Ushindi wowote kwa Azam FC dhidi ya Mbeya City, utaifanya kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa muda kwani itakuwa imefikisha jumla ya pointi 16, ambapo itakuwa ikisubiria matokeo ya wapinzani wake Simba, Yanga watakaokuwa wakichuana Oktoba 28 na Mtibwa Sugar itakayokipiga na Singida United.