KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuungana naye katika kuwasapoti wachezaji vijana anaoendelea kuwapa nafasi kikosini.

Azam FC msimu huu imekuwa na mchanganyiko wa wachezaji wengi vijana na wazoefu huku katika eneo la ushambuliaji ikiwa na changamoto kubwa kutokana na kuwa na wachezaji wengi vijana wanacheza kwa pamoja wanaohitaji muda kuweza kufanya vizuri.

Mabingwa hao jana walitoka sare ya tatu mfululizo kwenye mechi za ugenini za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kutoka suluhu na Mbao, mechi nyingine mbili za nyuma zikiwa dhidi ya Mwadui (!-1) na Singida United (1-1).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Cioaba ameweka wazi kuwa amepanga kuwapa nafasi wachezaji vijana na anaamini ya kuwa muda si mrefu watawapa mashabiki kile ambacho wanahitaji kutoka kwao cha muhimu ni kuwapa sapoti zaidi.

“Mechi ya jana dhidi ya Mbao imeisha kwa suluhu, dakika 45 za kwanza nilipata nafasi mbili hadi tatu, mashabiki wanatakiwa kutambua ya kuwa kwenye mechi na Mbao niliweza kuchezesha wachezaji wengi vijana, Razak ana miaka 20, Daniel 20, Yakubu 22, Enock 19, Idd 20, Zayd 20, Mbaraka ana miaka 21.

“Wachezaji wengi ni vijana na wengi hawana uzoefu, wachezaji hawa wanahitaji hali ya kujiamini ili kuweza kufanya vizuri, mashabiki waendelee kuwaamini, mechi imeisha kwa sare na lengo letu lilikuwa ni kuchukua pointi tatu, hivyo tutafanya kazi kubwa kuzidi kuwajenga hawa wachezaji vijana ili kuweza kuwa na makali kwenye ushambuliaji,” alisema.

Kocha huyo alisema licha ya kuwa na wachezaji wengi vijana, bado kikosi chake kimekuwa na mwenendo mzuri kwenye mechi saba za mwanzo walizocheza, ambapo hawajapoteza mchezo hata mmoja.

“Sisi tumejikusanyia pointi 13, waliokuwa juu yetu Simba, Yanga na Mtibwa Sugar wametuzidi pointi mbili tu, si jambo baya, tutaendelea kufanya kazi zaidi ya kukiboresha kikosi ili kuwa imara zaidi, cha muhimu ni mashabiki nao kuisapoti timu na kukaa karibu na wachezaji vijana kwa kuwapa moyo na kuwasapoti na hatua kwa hatua mabao yatakuja,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Nawaamini sana wachezaji vijana na natarajia kuwapa nafasi zaidi kwenye mechi zijazo ili kuwajenga zaidi.”

Aidha alisema kuelekea mchezo ujao dhidi ya Mbeya City, kikosi hicho kinatarajia kuerejea jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu na kufikia kambini moja kwa moja kujiandaa na mtanange huo unoatarajia kupigwa Ijumaa ijayo Oktoba 27 mwaka huu.

“Kuhusu mchezo ujao, tumekuwa na safari ndefu ya kurejea Dar es Salaam tumepitia hapa Dodoma kupumzika, kesho (Jumatatu) tutawasili Chamazi na wachezaji watafikia moja kwa moja kambini, tuatakuwa na maandalizi ya siku tatu kabla ya mchezo huo utakaofanyika Ijumaa,” alisema.