KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imemaliza mechi mbili za Kanda ya Ziwa jioni ya leo kwa kutoka suluhu dhidi ya Mbao katika mtanange wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kusogea kwa nafasi moja kwenye msimamo wa ligi hiyo ikikamata nafasi ya tatu kwa pointi 13, ikizidiwa pointi mbili na Mtibwa Sugar na Simba zilizo kileleni baada ya kufikisha pointi 15.

zikiwa zimeshachezwa raundi saba za ligi, Azam FC imefanikiwa kufunga mabao matano na kufungwa mawili tu ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja, na ndio timu pekee iliyoruhusu mabao machache ya kufungwa mpaka sasa.

Azam FC ilifanikiwa kucheza vizuri kwenye mchezo huo lakini tatizo kubwa lililoendelea kujionesha ni namna ya kuzitumia vema nafasi chache za kufunga mabao ilizozipata katika kila kipindi na namna ya washambuliaji kusetiana mipira ndani ya eneo 18.

Aidha katika mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC Aristica Cioaba, alibadilisha mbinu kwa kutumia mfumo wa 4-3-3 na kuachana na ule wa 3-5-2 alioutumia kwenye mechi nne zilizopita, na kufanikiwa kuibana vilivyo Mbao tofauti na namna zilivyocheza na timu nyingine ndani ya uwanja huo.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Mwanza kesho alfajiri na kitapata mapumziko mkoani Dodoma kabla ya keshokutwa Jumatatu kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kuanza maandalizi ya kuikabili Mbeya City katika mchezo ujao wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Ijumaa ijayo Oktoba 27.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Himid Mao (C), Idd Kipagwile/Ramadhan Singano dk 57, Salum Abubakar, Mbaraka Yusuph, Yahya Zayd/Yahaya Mohammed dk 72, Enock Atta/Wazir Junior dk 84