BAADA ya maandalizi ya takribani siku sita jijini hapa Mwanza, kikosi cha Azam FC kinatarajia kumenyana na wenyeji wao Mbao, katika mchezo unaotarajia kufanyika Uwanja wa CCM Kirumba kesho Jumamosi saa 10.00 jioni.

Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wengi wa mkoani Mwanza kutokana na ukubwa mchezo huo, ambapo kikosi cha Azam FC kimeendelea kujiimarisha kwa kufanya maandalizi makali kwa lengo moja tu la kuibuka na ushindi.

Wakati vikosi hivyo vikienda kukutana, zifuatazo ni baadhi ya dondoo muhimu kuhusu timu hizo:-

Ni vita ya kisasi

Moja ya mambo yatakayoibuka kwenye mchezo huo ni Azam FC kutaka kulipa kisasi cha msimu uliopita baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mtanange wa raundi ya kwanza ya ligi uliofanyika ndani ya dimba hilo.

Azam FC ilirejea vizuri kwenye mchezo wa marudiano raundi ya pili baada ya kuinyuka mabao 3-0 kwenye viunga vya Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Msimamo

Licha ya Azam FC kutoa sare mbili mfululizo kwenye mechi mbili zilizopita za ligi hiyo dhidi ya Singida United (1-1), Mwadui (1-1), mabingwa hao Afrika Mashariki na Kati ni miongoni mwa timu nne zinazochuana kileleni kuwania taji la ligi.

Azam FC ambayo imecheza mechi sita, tayari imejikusanyia jumla pointi 12 kwenye msimamo ikiwa nafasi ya nne, ikilingana pointi na timu tatu nyingine za juu Simba, Mtibwa Sugar na Yanga ambazo ziko juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Aidha Azam FC ndio timu pekee ambayo imefungwa mabao machache mpaka sasa ikiwa imeruhusu wake kuguswa mara mbili huku ikiwa haijaruhusu nyavu zake kuguswa (clean sheet) mara nne kati ya mechi sita ilizocheza.

Mbao yenyewe inashika nafasi tisa ikiwa imejisanyia jumla ya pointi sita baada ya kushinda mechi moja, sare mbili na kupoteza mchezo mmoja.

Kauli ya kocha Azam FC

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya mwisho leo jioni, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alisema kuwa kila mchezaji amefanya mazoezi kwa nguvu katika siku zote za maandalizi na kinachotakiwa ni kuingia uwanjani na kupambana na kushinda mtanange huo.

“Najua timu ya Mbao inacheza kwa nguvu ikiwa kwenye uwanja huu (CCM Kirumba), kama ikicheza na Azam inapenda kucheza kwa nguvu sana lakini nimejiandaa kwa mechi hii wachezaji wanatambua kuwa mechi ya kesho si nyepesi na wanatakiwa kuingia uwanjani na kupambana na kushinda mchezo,” alisema.