LIGI ya vijana chini ya umri wa miaka 15 ya Azam (Azam Youth League U-15) inatarajia kuingia katika wiki ya pili kesho Jumamosi asubuhi kwa mechi tatu kupigwa katika viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Wenyeji Azam U-15 wanaongoza ligi hiyo baada ya kuanza kwa kishindo kwa kuifunga Florida 6-0 Jumamosi iliyopita, watakipiga dhidi ya Rendis saa 4.30 asubuhi.

Rendis katika mchezo wake uliopita ilishinda 4-1 dhidi ya New Talent, ambayo imeondolewa kwenye michuano hiyo baada ya kushindwa kuthibitisha umri wa wachezaji wake na nafasi yake kuchukuliwa na Tanzanite ambayo inatokea Temeke, Dar es Salaam.

Mechi nyingine kesho, itashuhudiwa Tanzanite itakayocheza mechi yake ya kwanza baada ya kuchukua nafasi ya vijana wa Talents, ikikabiliana na JMK Park, ambayo kwenye mchezo wa kwanza iliilaza Bom Bom 4-2.

Florida iliyotoka kupewa kipigo kizito dhidi ya Azam U-15, itashuka tena dimbani kujiuliza pale itakapochuana na Bom Bom ambayo nayo imetoka kupoteza mchezo wa kwanza, zote zikiburuza mkia kwenye ligi hiyo.

#AYLU15 #Week2
#TimuBoraBidhaaBora
#MajiSafiNiUhaiDrinkingWater
#NMBKaribuYako
#Tradegents