KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imewatumia salamu wapinzani wao Mbao baada ya leo asubuhi kuichapa Copco FC mabao 6-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Mchezo huo ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya kikosi hicho kujiweka sawa kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mbao utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa Jumamosi hii.

Kocha Mkuu Aristica Cioaba, alichezesha vikosi viwili tofauti, kilichoanza kipindi cha kwanza kiliundwa na Mwadini Ally, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Frank Domayo, Enock Atta, Salum Abubakar, Mbaraka Yusuph, Yahya Zayd na Idd Kipagwile.

Kikosi kilichoingia kipindi cha pili kuliundwa na Benedict Haule, Swaleh Abdallah, Hamimu Karim, David Mwantika, Abdallah Kheri, Salmin Hoza, Braison Raphael, Ramadhan Singano, Yahaya Mohammed, Wazir Junior na Abdallah Masoud huku Yahaya akitoka dakika ya 76 na kuingia Paul Peter.

Azam FC iliweza kutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa kwenye kila kipindi, na kujipatia mabao matano kwenye kipindi cha kwanza yaliyofungwa na Enock Atta aliyepiga hat-trick, la kwanza akitupia dakika ya 9, la pili dakika ya 19 kwa njia ya adhabu ndogo ya moja kwa moja pembeni ya eneo la 18.

Winga huyo alikamilisha hat-trick yake dakika ya 40 akitupia bao safi la kiufundi, mabao mengine kipindi cha kwanza yalifungwa na washambuliaji Mbaraka Yusuph dakika ya 13, huku Yahya Zayd akitupia jingine dakika ya 36.

Kipindi cha pili Azam FC iliweza kutengeneza nafasi nyingi za kupata mabao lakini hazikutumiwa vema na washambuliaji wake, ambapo Yahaya alikosa takribani mabao manne ya wazi hadi anatolewa dakika ya 76.

Mshambuliaji Wazir Junior, ambaye naye alipoteza nafasi mbili, aliweza kuipatia Azam FC bao la sita dakika ya 88 kwa jitihada binafsi akiwazidi maarifa mabeki kabla ya kutupia.