NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuwapa moyo na kuwaunga mkono wachezaji vijana ndani ya kikosi hicho.

Kauli ya Mao imekuja siku chache mara baada ya mashabiki kuanza kuwalaumu na kuwakosoa wachezaji vijana walioanza kuaminiwa na kupewa nafasi ndani ya kikosi hicho kama vile washambuliaji Mbaraka Yusuph na Yahya Zayd.

Mao ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa si jambo zuri kuanza kuwalaumu wachezaji hao bali ni vema wakaungwa mkono ili baadaye waweze kuwa wachezaji bora.

“Ukiangalia timu yetu msimu huu ina wachezaji wengi wapya na wengi wao hawana uzoefu, kuwakosoa labda au kuwasema vibaya kuhusu wao si kitu kizuri sana na si busara sana kwa sababu wanahitaji muda wacheze na waweze kukua kimchezo na baadaye waweze kuwa wachezaji tegemezi wa Azam FC na Taifa kiujumla.

“Nafikiri kitu kizuri zaidi ni kuwapa moyo hata wanapokosea, kuwaunga mkono ili waje kuwa wachezaji bora kwa sababu hata sisi tulipoanza tulikuwa wadogo sana hatukuvunjwa moyo tulipewa sapoti kubwa tuliyoihitaji hadi leo tumekuja kuwa wachezaji tunategemewa kwenye timu kwa hiyo naamini hata hawa wachezaji waliokuwepo pia, wapya wanahitaji hicho kitu kuwajenga na kuwa wachezaji wazuri baadaye,” alisema

Azam FC imekuwa na utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi wachezaji vijana msimu huu Kocha Mkuu Aristica Cioaba, ikiwapandisha Zayd, Stanslaus Ladislaus, Paul Peter kutoka timu yake ya vijana chini ya miaka 20 (Azam FC U-20).

Mara baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui juzi, tayari kikosi cha Azam FC kimewasili mkoani Mwanza kwa mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ugenini, ikikipiga dhidi ya Mbao katika Uwanja wa CCM Kirumba Jumamosi hii.