KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeenda sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Mwadui, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika  leo Uwanja wa Mwadui Complex.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 12 katika nafasi ya pili kwenye msimamo sawa na Yanga iliyokileleni kwa tofauti ya mabao kufunga.

Bao pekee la Azam FC limefungwa dakika ya tisa na nahodha Himid Mao ‘Ninja, kwa njia ya mkwaju wa penalti baada ya beki wa kushoto Bruce Kangwa, kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

Azam FC ingeweza kujipatia mabao zaidi ya mawili katika kipindi cha kwanza, kama washambuliaji wake chipukizi, Yahya Zayd na Mbaraka Yusuph wanegkuwa makini kutumia nafasi takribani tatu za kufunga mabao.

Mwadui iliweza kujipatia bao la kusawazisha dakika ya 80 kupitia kwa winga wake, Hassan Kabunda, aliyefunga kwa kichwa  na kufanya timu zote kuzoa pointi moja.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuelekea mkoani Mwanza kesho Jumapili saa 2 asubuhi tayari kabisa kuanza maandalizi ya kuivaa Mbao katika mtanange mwingine wa ugenini utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba Oktoba 21 mwaka huu.