LIGI ya Vijana ya Azam chini ya umri wa miaka 15 (Azam U-15 League) inatarajia kuanza kutimua vumbi kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Michuano hiyo iliyoandaliwa na Azam FC kwa kushirikiana na Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, ni ya tatu kuandaliwa na timu hiyo, baada ya ile ya Afrika Mashariki ya chini ya umri wa miaka 20 mwaka jana, chini ya miaka 13 Juni mwaka huu (Azam U-13 League).

Jumla ya timu sita sita zinatarajia kushiriki kwenye michuano hiyo itakayochukua jumla ya wiki 10 ikifanyika kila Jumamosi ya wiki, ambazo ni wenyeji Azam FC, JMK Park Academy, Florida Academy, Rendis Academy, New Talent Academy na Bom Bom SC.

Mashabiki watakaohudhuria ufunguzi wa michuano hiyo wanatarajia kushuhudia mechi tatu mechi tatu kali, wenyeji Azam wakianza kukipiga na Florida saa 2.30 asubuhi, kabla ya Rendis kuvaana na New Talent saa 3.30 asubuhi huku mechi ya kufunga dimba kwa kesho ikitarajia kuwakutanisha JMK Park na Bom Bom saa 4.30 asubuhi.

Sheria za michuano hiyo;

*Sheria ya kwanza ya michuno hiyo inahusu muda wa mchezo, ambapo kila mchezo utachukua dakika 60; dakika 30 katika kila kipindi.

*Kama kawaida sheria za kurusha mipira (throw ins) na mtu kuotea (offsides) zitakuwepo.

*Timu ni lazima zibadilishe wachezaji wasiopungua watatu kutoka katika kikosi chao kilichoanza kwenye mchezo uliopita, hii ni katika kusaidia maendeleo ya wachezaji kikosini.

*Sheria ya mwisho, hakuna kocha atakayeruhusiwa kukaa kwenye benchi badala yake watakaa majukwaani.

Pia makocha hawataruhusiwa kabisa kuongea na wachezaji wao wakati mchezo ukiendelea bali wataruhusiwa kuongea nao kabla ya mchezo, wakati wa mapumziko na mwisho wa mchezo.

Hiyo ni katika kusaidia wachezaji kufanya maamuzi wakati wa mchezo bila ushswishi wa kocha. Inatakiwa kuwajenga wachezaji ambao watakuwa wakifanya maamuzi kupitia akili yao kuliko kuwa kama roboti kusikiliza maamuzi ya kocha kwenye benchi.