KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimewasili salama mkoani Shinyanga jioni hii kikiwa na morali kubwa ya kuibuka na ushindi dhidi ya Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) unaotarajia kufanyika Jumamosi hii.

Azam FC imewasili ikiwa na kikosi kamili isipokuwa kiungo Stephan Kingue, ambaye bado hajapona vizuri majeraha ya mgongo, ambapo kabla ya kikosi hiki kutua hapa jana kilipumzika mkoani Dodoma na kufanya mazoezi jioni kwenye Uwanja wa Gadafi.

Kikosi hicho kikiwa hapa mkoani Shiyanga kimefikia katika Hoteli ya Vigimark, ambapo kwa mujibu wa programu ya kocha kesho ndio kitafanya mazoezi ya kwanza mkoani humu tayari kabisa kumalizia sehemu ya maandalizi ya kuwavaa Mwadui, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mwadui Complex.