BAADA ya kinda wa timu ya vijana ya Azam FC (Azam U-20), Paul Peter, kufanya vema na timu ya wakubwa mkoani Dodoma, Kocha Mkuu wa timu hiyo Aristica Cioaba, amesema kuwa anatarajia kuwatambulisha vijana wengi zaidi katika kikosi chake watakaokuwa wakifanya vizuri kwenye Azam Academy.

Peter aliyepandishwa kwenye kikosi hicho Jumanne iliyopita, alitumia siku nne tu mazoezi na kikosi cha wakubwa kuweza kutangaza vema jina lake kwa kufunga bao la kusawazisha na Azam FC kuvuna pointi moja dhidi ya Singida United juzi Jumamosi kwenye sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Cioaba alisema amekuwa na programu nzuri ya kufuatilia maendeleo ya kikosi hicho cha vijana kwenye baadhi ya mechi ili kuwamulika wachezaji watakaokuwa wakifanya vizuri na hatimaye kuwapa fursa katika timu kubwa (Azam FC).

“Paul (Peter) ni mshambuliaji mzuri kijana, licha ya uchanga wake haikunipa shida mimi kama kocha kuweza kumpa nafasi kwenye mechi iliyopita, angalia alivyoingia aliweza kupambana na hatimaye kuitumia vema nafasi moja aliyoipata kufunga bao muhimu, hili ni jambo zuri sana kwa klabu kuwa na vijana wa aina ya Paul, ninafuraha pia kusikia ameitwa timu ya Taifa ya Vijana (Ngorongoro Heroes), naamini atawafungulia njia wachezaji wengine wa Azam B kupata nafasi hii kama yake.

“Mimi ni kocha ninayependa wachezaji vijana, nimepanga kuendelea na njia hii ya kuwapa hamasa wachezaji vijana kwa kuwajumuisha kwenye timu kubwa, sitajiuliza mara mbili pale ninapoona mchezaji mzuri kwenye timu ya vijana (Azam B) hasa ninapoona anaouwezo wa kuisaidia timu kubwa, bado kuna wachezaji wengine nawafuatilia zaidi, kama wakiendelea na mwenendo wao mzuri wa kujitahidi kwenye mechi, kufanya mazoezi kwa bidii na kupambana uwanjani kwa hakika nao watapata nafasi hii,” alisema kocha huyo kwa msisitizo.

Kocha huyo pia aliwaomba mashabiki na watu wote kuwapa sapoti na kuwavumilia wachezaji vijana kila wanapopewa nafasi hata pale wanapokuwa hawatoi kile kinachotarajiwa kwani ndio fursa yao ya kujifunza kupitia ushindani mwingine wa hali ya juu tofauti ya ule wa ngazi ya chini waliokuwa wakikutana nao awali.

Cioaba amekuwa na mfumo mzuri wa kuwajenga wachezaji vijana na kuwapa nafasi kwenye kikosi chake, mpaka sasa ingizo la Peter linakuwa ni la sita kwenye kikosi cha wakubwa baada ya kuwapa nafasi mshambuliaji Yahya Zayd, Shaaban Idd, viungo Braison Raphael, Stanslaus Ladislaus na beki wa kulia Abdul Omary ‘Hama Hama’, ambaye amekuwa akimuandaa kwa hapo baadaye kuwa tegemeo kwenye kikosi hicho.