MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Paul Peter, ameahidi kufanya makubwa zaidi kwenye klabu hiyo katika mechi zijazo.

Kauli hiyo imekuja mara baada ya kinda huyo kuifungia bao la kusawazisha Azam FC na kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida United jana, ikiwa ni mechi yake ya kwanza kucheza tokea apandishwe kutoka timu ya vijana (Azam B) Jumanne iliyopita.

Ilimchukua dakika tatu tu kinda huyo kuweza kufunga bao hilo dakika ya 87 baada ya kutokea benchi dakika ya 84 akichukua nafasi ya mkongwe Yahaya Mohammed.

Aliahidi kufanya kweli vs Singida

Wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kabla ya mchezo huo Peter aliwaahidi mashabiki kufanya kweli kwenye mchezo kama angepewa nafasi ya kucheza, na kweli aliweza kutimiza hilo kwa kuipatia Azam FC pointi hiyo moja baada ya kuifungia bao muhimu.

“Nawaahidi mambo mazuri mashabiki Inshallah kama leo (jana) nikipangwa, nikicheza naahidi mambo mazuri na mechi zijazo,” alisema kabla ya mchezo huo.

Katika mahojiano mengine mara baada ya mchezo huo, Peter amemshukuru kocha Aristica Cioaba kwa kumpa nafasi ya kucheza huku akidai mwanzo alipata hofu, lakini aliweza kuiondoa na kufanya kweli alipoingia uwanjani.

“Kwanza namshukuru Mungu, pili naushukuru uongozi mzima wa Azam FC tatu namshukuru sana Mama yangu, nashukuru kwa kufanikisha kufunga goli na kuipatia timu yangu pointi moja,” alisema.

Kujua alichoongea zaidi Paul Peter fuatilia video, kwenye chaneli yetu ya YouTube: https://youtu.be/ukVsn5PSBbU