KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeondoka na pointi moja kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika leo jioni.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kuendelea kukaa kwenye nafasi mbili za juu katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha jumla ya pointi 11 sawa na Mtibwa Sugar iliyokileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Alikuwa ni kinda Peter Paul, aliyefanya mazoezi ya siku nne na kikosi hicho baada ya kujumuishwa kwenye timu kubwa akitokea timu ya vijana ya Azam FC (Azam U-20), ambapo aliweza kuipatia bao la kusawazisha timu hiyo dakika ya 87 kwa shuti la kiufundi.

Ilimchukua dakika tatu tu kinda huyo kuweza kuandika rekodi hiyo muhimu katika historia yake ya soka ya kuipatia bao hilo Azam FC baada ya kutokea benchi dakika ya 84 akichukua nafasi ya mkongwe Yahaya Mohammed.

Singida United ilitangulia kupata bao la uongozi dakika ya 39 kupitia kwa mshambuliaji wao, Danny Usengimana, bao ambalo lina utata kutokana na marudio ya kwenye televisheni kuonyesha mfungaji alikuwa ameotea kabla ya kufunga.

Bao hilo lilihitimisha rekodi ya Azam FC ya kucheza mechi nne sawa na dakika 360 bila kuruhusu wavu wake kuguswa, hata hivyo ikiwa ndio timu pekee iliyofungwa bao moja tu hadi sasa kwenye ligi hiyo.

Kwa hakika ubovu wa uwanja nao ulichangia kuondoa ladha ya mpira huo, kutokana na udongo kuwa mgumu na vumbi kutimka kila mara hali ambayo ilizilazimu timu zote mbili kutumia mipira mirefu katika kujenga mashambulizi.

Azam FC ilionekana kucheza vema kipindi cha pili tofauti na kipindi cha kwanza, hasa baada ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba kuwaingiza washambuliaji wenye kasi Yahya Zayd, Idd Kipagwile na mfungaji wa bao Paul, ambao waliongeza uhai katika eneo la ushambuliaji wakishirikiana na Mbaraka Yusuph.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumapili, tayari kabisa kuivutia kasi Mwadui katika mtanange ujao utakaofanyika Uwanja wa Mwadui, Oktoba 14 mwaka huu mara baada ya kumalizika kwa wiki ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora, Daniel Amoah, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Swaleh Abdallah/Idd Kipagwile dk 86, Bruce Kangwa, Himid Mao (C), Braison Raphael/Yahya Zayd dk 65, Salum Abubakar, Yahaya Mohammed/Peter Paul dk 84, Mbaraka Yusuph