WAKATI ikiwa imesalia siku moja kabla ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, haijavaana na Singida United kesho Jumamosi zifuatazo ni siku 35 za awali za timu hiyo kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Azam FC ipo kamili kabisa kuelekea mchezo huo, wachezaji wakiwa na morali kubwa kuhakikisha wanavuna pointi zote tatu na kuendelea kabakia nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Ngumu kufungika

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa inajivunia rekodi ya kucheza mechi nne za ligi hiyo sawa na dakika 360 bila kuruhusu wavu wake kuguswa na kuwa ndio timu pekee kufanya hivyo msimu huu.

Ubora huo unadhihirishwa na safu nzuri ya eneo la ulinzi iliyokuwa nayo, langoni akiwa kipa boa kabisa Razak Abalora kutoka Ghana ambaye hadi anasajiliwa na Azam FC msimu huu alikuwa hajafungwa bao kwenye 14 za Ligi Kuu Ghana akiwa na timu ya WAFA SC.

Kipa huyo analindwa na safu nzuri ya mabeki wa kati chini ya nahodha msaidizi Agrey Moris, Yakubu Mohamed, mabeki wa pembeni Bruce Kangwa na Daniel Amoah, wakiwa wanashirikiana vema na viungo nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Stephan Kingue, Frank Domayo ‘Chumvi’ na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Mfumo wa kasi

Moja ya staili nyingine ya mchezo inayoibeba Azam FC msimu huu ni uwezo mkubwa wa kucheza soka la kasi inaposhambulia, ambalo limekuwa likiwapa wakati mgumu timu pinzani ikinufaika na unyumbulikaji wa washambuliaji chipukizi Yahya Zayd na Mbaraka Yusuph wakisaidiana na mkongwe Yahaya Mohammed.

Yusuph katika mechi mbili zilizopita dhidi ya timu yake ya zamani Kagera Sugar na Lipuli, ndiye amefunga mabao pekee ya Azam FC kwenye ushindi wa bao 1-0, mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Zayd aliyepandishwa kutoka Azam B na Yusuph ni washambuliaji wapya walioingia kwenye timu hiyo msimu huu, hivyo wanahitaji muda ili kuweza kufanya kile ambacho mashabiki wengi wa Azam FC wanakitarajia.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amekuwa mjanja wa mbinu kwa kiasi kikubwa akibadilika mchezo hadi mchezo akilindwa na mifumo yake miwili 4-3-3 na 3-5-2, na imekuwa ni ngumu kwa timu pinzani kuizidi maarifa timu hiyo kwa asilimia kubwa mchezoni.

Ushindi kipindi cha kwanza  

Takwimu za Azam FC zinaonyesha kuwa katika mechi nne walizocheza na kufunga mabao matatu, imekuwa ndio timu pekee ambayo imeweza kupata ushindi wake ndani ya kipindi cha kwanza cha mchezo na kuulinda hadi mwisho wa dakika 90.

Ni mechi moja tu msimu huu dhidi ya Simba, ambayo Azam FC haikuweza kufunga bao iliyoisha kwa suluhu ikifanyika Uwanja wa Azam Complex, iliyokuwa mechi ya kihistoria kwa matajiri hao wa Chamazi kucheza na Wanamsimbazi hao katika uwanja wake wa nyumbani kwenye mechi rasmi huku Yanga nayo ikitarajia kuchezea hapo kwa mara ya kwanza.

Msimamo VPL

Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Tradegents, itaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo kwa pointi 10 ilizojikusanyia sawa na Mtibwa Sugar, ambayo ipo kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Singida United yenyewe ipo katika nafasi ya tatu kwa pointi tisa ilizojisanyia baada kushinda mechi tatu na kufungwa mchezo mmoja.

Cioaba vs Pluijm

Mchezo huo wa kesho utawakutanisha makocha wawili wanaofahamiana vema kufuatia kila mmoja kuwahi kufanya kazi nchini Ghana miaka michache iliyopita, Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba na Mholanzi Hans van Pluijm wa Singida United.

Hivyo mbali na vita ya uwanjani, pia mchezo huo unatarajia kunogeshwa na upinzani wa wawili hao waliotoka nao nchini Ghana, ambapo kila mmoja atataka kumtambia mwenzake kwa kukiwezesha kikosi chake kuibuka na ushindi.

Cioaba ameweka wazi kuwa licha ya uwanja wa Jamhuri kutokuwa katika hali nzuri, amekipanga kikosi chake kimbinu kuweza kuibuka na ushindi.

“Timu imewasili hapa (Dodoma) siku mbili kabla ya mchezo, iko tayari kwa ajili ya mchezo huo tatizo moja tu linalotukabili ni uwanja, huyu ni mpinzani mkubwa kwa upande wetu wa Azam FC, timu inatarajia kufanya mazoezi leo (Ijumaa) kwenye uwanja huo ili kuuzoea, na inahitaji mbinu nzuri kwenye mchezo huo ili kubeba pointi zote tatu.

“Kama wachezaji watanisikiliza kwa kile nilichowafundisha kwa ajili ya kukifanya uwanjani kwenye mchezo huo inwezekana kushinda na kuzoa pointi zote tatu, lakini kama wachezaji wataingia uwanjani na kutoweka umakini kwa kile nilichowafundisha basi itakuwa ni tatizo kwa upande wetu,” alisema Cioaba.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana kwenye Ligi Kuu, ambapo timu yoyote itakayoibuka kidedea ina nafasi kubwa ya kukaa kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo inatarajia kusimama kwa wiki mbili baada ya wikiendi hii kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambapo Tanzania ‘Taifa Stars’ ikitarajia kukipiga na Malawi.